Injili ya Mungu

Injili ya Mungu

Paulo anaeleza injili ya Mungu: Yesu ni nani kwa jinsi ya mwili, na Yeye ni nani kwa jinsi ya Roho.

17/11/2026—5 dk

Written by Sigurd Bratlie

Injili ya Mungu

“Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu, Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu, yaani Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi, na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani Yesu Kristo, Bwana wetu.” Warumi 1:1-4.

Manabii katika Agano la Kale walitabiri kuhusu Yesu katika Isaya 7:14-15, katika Isaya 9 na katika Isaya 53. Pia tunasoma kumhusu katika Mika 5, na katika sehemu nyingine nyingi sana. Katika Agano Jipya tunaweza kupata unabii kumhusu katika Luka 24:26-27, Matendo 18:28, 1 Petro 1:10-13, na sehemu nyingine.

Katika Warumi 1:1-4, Paulo anaeleza kwa ufupi Injili ya Mungu kuhusu Yesu katika sehemu mbili: Yeye ni nani kwa jinsi ya mwili, na Yeye ni nani kwa jinsi ya Roho. Tukiondoa au kubadilisha mojawapo ya sehemu hizi, basi haitakuwa tena Injili ya Mungu.

Inamaanisha nini kwamba alikuwa mzao wa Daudi kwa jinsi ya mwili? Inamaanisha hasa kile inachosema. Tunajua kuhusu Daudi na wazao wake. Paulo alikuwa wa watu haohao (Waebrania 2:16). Paulo anasema hivi kujihusu, “Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote linalokaa ndani yangu, yaani katika asili yangu ya dhambi.” Warumi 7:18. Kwa hiyo huu ndio ulikuwa mwili, yaani asili ya kibinadamu, aliyokuwa nayo Yesu.

Yesu “alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu … kwa uwezo wa Roho wa utakatifu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu”. Hili pia hatuwezi kulibadilisha. Kwa hiyo swali ni: Alipokuja duniani katika mwili uliotokana na uzao wa Daudi, je, alileta pamoja naye utimilifu wote wa Mungu katika Roho wake? Jibu ni “Hapana,” kwa sababu imeandikwa, “… Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kushikilia, bali alijifanya si kitu, akachukua hali hasa ya mtumwa, naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akatii hata mauti: naam, mauti ya msalaba!” Wafilipi 2:6-8.

Mara nyingi husemwa kwamba alikuwa Mungu wa kweli na Mwanadamu wa kweli. Lakini hilo si kweli ikiwa hilo lingemaanisha kwamba alikuja na utimilifu wote wa Mungu pamoja naye alipokuja duniani katika mwili uliotokana na ukoo wa Daudi. Na hilo pia haliendani tunaposoma Waebrania 12:2, “… Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu.”

Soma zaidi hapa: Kwa nini Yesu alilazimika kufa msalabani?

Yaliyotokea ndani ya Yesu katika siku za maisha yake hapa duniani

Katika Waebrania 5:7-10 tunasoma, “Katika siku za maisha ya Yesu hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu. Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata, naye akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii. Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.”

Tunasoma kwamba maombi yake yalisikiwa. Basi haingeweza kuwa kifo chake msalabani Kalvari alichoomba aokolewe nacho, kwa maana ilimbidi kuteseka kifo hicho ili kupatanisha vitu vyote na Mungu (Wakolosai 1:19-22; 2 Wakorintho 5:19).

“Kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa …” Warumi 8:13. Ilikuwa ni kwa sababu ya kifo hiki ndipo aliomba kwa kilio kikuu na machozi kwake yeye awezaye kumwokoa na mauti. Maombi yake yalisikiwa, na kifo hakingeweza kumzuia. Hapa tena tunaona sehemu zote mbili za injili.

Katika Waebrania 2:14-15 tunasoma, “Basi kwa kuwa watoto wana mwili na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti.”

Tunasoma katika Mwanzo jinsi nyoka alivyomdanganya Hawa na kumwambia kwamba angekuwa kama Mungu na kujua mema na mabaya. Alimjaribu Hawa kwa utukufu ambao alisema angeweza kuupata kwa kutotii; lakini matokeo yake yalikuwa mauti. Yesu alikuja kwanza na mauti, na kupitia mauti akamwangamiza yule aliyekuwa na mamlaka ya mauti. Alikuja na mauti dhidi ya tamaa na matamanio, ambayo ndiyo chanzo cha uharibifu wote duniani na ambayo huishia katika mauti (2 Petro 1:4). Lakini kupitia mauti ambayo Yesu alikuja nayo, tunafikia—kwa njia ya utii—utukufu ule ambao nyoka alimshawishi Hawa kuupata.

Karibu kila mtu anaamini uongo uleule ambao Hawa aliamini, na huishia katika uharibifu. Lakini Yesu alikuja na mauti dhidi ya tamaa na matamanio, akamwangamiza ibilisi aliyekuwa na nguvu za mauti; na kwa wale wanaoamini, nguvu za ibilisi pia zimeangamizwa. Hili lilithibitishwa Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu. Paulo alikuwa ameamini hili, na kupitia ufahamu huu wa Yesu angeweza kusema, “Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.” Wafilipi 1:21-23.

“Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili,” Warumi 8:3. Hii ilikuwa sehemu ya kwanza ya injili, na ilifanya sehemu ya pili iwezekane.

Warumi 8:3 ndio msingi wa injili, na katika Warumi 8:4 tunasoma kile injili ilicho: “… ili haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.”

Chapisho hili linapatikana katika

Makala hii imetafsiriwa kutoka Kinorwe na ni toleo lililofupishwa kidogo la sura mbili za kwanza za kitabu “Injili ya Mungu,” kilichochapishwa kwa mara ya kwanza na Skjulte Skatters Forlag mnamo Januari 1988. Imebadilishwa kwa idhini kwa matumizi katika tovuti hii.

© Hakimiliki Stiftelsen Skjulte Skatters Forlag