Je, ninahitaji kuogopa ugaidi?

Je, ninahitaji kuogopa ugaidi?

Kwa nini nisiogope katika nyakati hizi zisizo na uhakika? Neno la Mungu linasema nini kuhusu hili?

29/8/20165 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Je, ninahitaji kuogopa ugaidi?

Inaonekana kama vyombo vya habari vimejaa habari kuhusu mashambulizi ya kigaidi. Inaonekana kutokea mara nyingi zaidi sasa, na huwezi kujua ni wapi itatokea baadaye. Treni, maduka makubwa, masoko, maeneo ambayo ni karibu sana na nyumbani, ni shabaha za wapiga risasi na washambuliaji wa kujitoa muhanga.

Nikisikiliza habari, mara nyingi huwa nashtuka, na inanifanya nihuzunike na kuniogopesha. Ninawahurumia sana wale ambao wamepoteza wapendwa wao, na mawazo ya wasiwasi na hofu huleta machafuko ndani yangu. Je, wapendwa wangu au mimi mwenyewe tutakuwa wahanga wanaofuata?

Ninajua kwamba magaidi hueneza hofu, ugaidi na kutokuwa na uhakika kama njia yao ya kupata kile wanachotaka. Nikishindwa na woga, maana yake ninakwenda sambamba na mipango yao. Lakini ninawezaje kuto-kuogopa?

Kupekua katika Biblia, nilipata ahadi nyingi zenye nguvu na mistari iliyojaa faraja. Lakini mstari mmoja, haswa, ulinisaidia sana.

Yesu amelitatua

Nami nawaambia ninyi marafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi… Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.” Luka 12:4-7

Maneno ya Yesu mwenyewe kutoka miaka 2000 iliyopita bado yanatumika leo na kunipa jibu wakati nilipohitaji. Alichukiwa na kuteswa wakati wake hapa duniani. Lakini katikati ya haya, alijua kwamba Mungu alikuwa na mpango mzuri kwa ajili Yake, na kwa ajili yetu sisi ambao tungemfuata.

Ni kana kwamba alijua jinsi ninavyosahau kwa urahisi na ninahitaji kukumbushwa. Ili atuokoe, alijitwalia mwili uleule wa dhambi kama tulio nao (Warumi 6:6) na alijaribiwa kama sisi. Yeye binafsi aliteseka, akashinda dhambi, alituwekea kielelezo, na kufungua njia ya kurudi kwa Baba yetu wa mbinguni. Na Yesu alijua kwa hakika kwamba wale wanaomwamini wanaweza kufuata mfano wake, na kushiriki umilele pamoja Naye. Kwa hiyo, alitufariji kwa kusema kwamba kifo si kitu cha kuogopa.

Tayari alikuwa amefikiria juu ya wasiwasi wangu, na Alinipa jibu nililohitaji.

Uaminifu usiotetereka

Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote…” Luka 12:7. Yesu lazima alipitia haya tena na tena. Ulimwengu uliomzunguka haukuwa na uhakika sana. Kundi la watu lilimwabudu kama Mwana wa Mungu, lakini punde baadaye watu wale wale walichochewa kumchukia sana hivi kwamba walitaka auawe msalabani. Katika mambo haya yote, Alimwamini Mungu na kujifunza kusema Hapana kwa mapenzi yake, akimtii Mungu badala yake.

Yesu alimtumaini Mungu kabisa, badala ya kutumainia nguvu na ufahamu wake mwenyewe. Alijifunza kwamba hakuna mtu angeweza kumdhuru isipokuwa Mungu aruhusu. Mungu alikuwa Baba yake ambaye alimjali kwa kweli katika hali zote za maisha. Alikuwa mtiifu kwa mapenzi yote ya Mungu, akiwa na uhakika kabisa kwamba Mungu ndiye anayetawala, na hilo lilimpa amani kuu! Sasa ameinuliwa, na kuketi mkono wa kuume wa Mungu, na anatuombea. (Warumi 8:34 ) Anasali kwamba niweze pia kumtumaini Mungu na kupata amani ileile isiyotikisika na tumaini lilelile la uzima wa milele.

Chochote kitatokea…

Mtume Paulo alikuwa mtu ambaye aliacha kila kitu ili kupata maisha sawa na Kristo. Pia alikabili nyakati ngumu akiwa na imani isiyotikisika.

Katika kila aina ya hali ngumu, daima alipata fursa za kutoa mwili wake “kama dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu”. Warumi 12:1. Alikaa katika upendo, na aliendelea kuvumilia mambo yote, kuamini mambo yote, kutumaini mambo yote na kustahimili mambo yote. (1 Wakorintho 13.)

Ni lazima pia awe amejaribiwa kuwa na wasiwasi, woga, kuvunjika moyo na uchungu. Alipata kila aina ya shida, lakini hakukandamizwa, anasema. Aliona hali hizi kuwa fursa za kupata utukufu wa milele na, badala ya kukubali, alisema Hapana kwa dhambi ambayo alijaribiwa nayo na kushinda. Aliandika, “Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu , yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana.” 2 Wakorintho 4:17.

Badala ya kuwa na wasiwasi kwamba “mambo haya mabaya yanaweza kunipata,” je, sipaswi kufurahishwa na ukweli kwamba ninaweza kushinda kitu cha milele katika kila hali ninayoingia leo? Ninaweza kushinda kutoamini, kuvunjika moyo, wasiwasi, na ninaweza kukaa katika upendo na matumaini, chochote kitakachotokea. Hivi ndivyo ninavyoweza kupata matunda ya Roho kama vile subira, wema, amani na furaha, na utukufu wa milele ambao Mungu ameniandalia.

Mungu ndiye anayetawala

Kwa sasa dunia inaonekana giza. Maneno kama vile "vitisho", "ugaidi", na "mauaji" mara nyingi huwa kwenye habari. Watu wanakufa na kuteseka. Najua hakuna maneno yanayoweza kuelezea mshtuko na maumivu ambayo waathiriwa na familia zao wanapitia. Ninapotumia Neno la Mungu kujenga imani yangu, mimi pia huwaombea kwa unyoofu.

Yesu ametuonya kuhusu nyakati hizi za kutisha tunazokabili. "Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme," ambayo ni "mwanzo wa huzuni". Uasi-sheria utaongezeka zaidi na zaidi kabla Kristo hajarudi. ( Mathayo 24:6-14 )

Mambo mengi yanayotokea sasa hayawezi kueleweka. Lakini Mungu aliahidi kwamba huzuni na maovu yote katika ulimwengu huu yatakwisha. Yesu atarudi ili kuharibu uovu wote, na Ufalme wake wa amani hautaisha. ( Isaya 9:7 ) Kuhusu wale wanaoleta uharibifu na uovu huu duniani, Mungu asema waziwazi mwisho wao utakuwa nini. "Mwisho wa mwenye dhambi ni uharibifu." Zaburi 1:6.

Ingawa wengi wanapigana dhidi ya ugaidi kwa njia zao wenyewe, ninaweza kupigana na hofu katika maisha yangu mwenyewe. Biblia haiahidi kwamba mimi au mtu ninayempenda hataathiriwa kamwe na ugaidi, au janga jingine lolote lisiyotarajiwa maishani. Lakini inaahidi kwamba ninaweza kumfuata Kristo, haijalishi jinsi ulimwengu unavyobadilika au chochote kinachonipata.

Nikiwa na Mungu upande wangu, sitakubali kamwe kuingiwa na woga, chuki, mashaka au ukosefu wa fadhili ambao utaleta tu kutokuwa na uhakika au uharibifu zaidi katika ulimwengu huu.

Chapisho hili linapatikana katika

Makala haya yanatokana na makala ya Bessie Wong iliyochapishwa awali kwenye https://activechristianity.org/ na yamebadilishwa kwa ruhusa ya matumizi kwenye tovuti hii.