“Basi kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani katika utauwa wote na ustahivu.” 1Timotheo 2:1-2.
Mtume Paulo anatwambia kwamba tunapaswa kuwaombea watu wote. Hii inamaanisha pia kwa watawala wa nchi yetu. Tunapotazama siasa na watu waliopo kwenye mamlaka na wale wanaotaka kuingia madarakani, inaweza onekana kama kazi isiyo na maana. Itasaidia nini hata kama nikiwaombea viongozi ambao wanaweza wasiwe watauwa na wenye majivuno, viongozi ambao hawako tayari hata kumsikiliza Mungu? Itasaidia nini kuwaombea na tuwaombee kwa lipi hasa? Lengo kuu hasa la kuomba tunaloambiwa kwenye kifungu hiki ni lipi?
Paulo alijua kwamba Mungu husikia maombi ya watu wanaomwogopa Mungu na wenye haki. Yakobo anaandika kuhusu Eliya: “Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidi. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidi mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.” Yakobo 5:16-18.
Watu wenye hofu ya Mungu hawapaswi tu kutofanya chochote na kukubali chochote kinachoweza kuja. Tunapaswa kuwaombea viongozi wetu na nchi yetu kwa bidi! Haijalishi kiongozi ni mtu wa aina gani. Tunasoma katika Mithali 21:1: “Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA; kama mifereji yam aji huugeuza po pote apendako.”
Mungu huitazama dunia nzima kutafuta wale waliojitoa moja kwa moja kwa ajili yake ili awasaidie. (2 Mambo ya nyakati 16:9) Yakobo anasema: “Wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!” Paulo anayaambia makanisa kuwaombea waliopo katika utawala ili Mungu awape hekima kuiongoza nchi katika namna ambayo tunaweza kumtumikia yeye katika amani. Tunapaswa kusimamia kile kilicho haki katika ulimwengu usio wa kitauwa; Tusipoiombea serikali na kwa kile kilicho haki, nani ataomba?
Tunafahamu kwamba Mungu ana nguvu na anaweza kufanya lolote analotaka kufanya. Lakini hatupaswi kutofanya chochote na kukubali kila kitu kwa sababu hiyo. Kuna mifano katika biblia ambapo Mungu alibadili mipango yake kwa sababu ya watu walioomba. Aliamua kuiangamiza Israeli baada ya kutenda dhambi ya kujichongea ndama wa dhahabu na kumwabudu, lakini Musa alimsihi na Kumwomba Mungu kwa ajili ya Israel, na Mungu alimsikia Musa na kuliacha taifa. (Kutoka 32:11-14)
Kwa hiyo, tunapaswa kufanya alichoandika Paulo na tuwaombee viongozi wetu na kumwomba Mungu aongoze njia zao. Tunaweza kumwomba Mungu kubadili mambo ili tuweze “kuwa na maisha tulivu na ya amani yaliyojazwa heshima na kumwabudu Mungu”. Kwa mfano, tunaweza kuomba kwamba hakuna sheria ambazo zinatungwa na serikali ambazo zitatuzuia sisi kukutana pamoja kama wakristo au itafanya ugumu wa kuishi kama wakristo. Tunaweza kumwomba Mungu kuilinda nchi yetu kwa ajili ya familia zetu na wapendwa wetu.
Tunaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu husikia maombi yetu kwa ukaribu, na hubadili mambo yote katika nchi yetu.