Sigurd Bratlie (1905-1996) alikuwa kiongozi wa Kanisa la kikristo la Brunstad kuanzia mwaka 1976 hadi kifo chake mwaka 1996. Alikuwa na uwezo wa pekee wa kuelezea injili na mafundisho ya mitume kwa njia iliyo wazi na rahisi, kiasi kwamba kila mtu angeweza kuelewa. Alikuwa na upendo wa kweli kwa watu na aliishi kwa haki mbele za Mungu, akiweka kweli alizohubiri katika matendo katika maisha yake mwenyewe.
Bratlie alihisi huzuni kuu na hasira ya haki juu ya mafundisho ya juu juu ambayo mara nyingi yaligeuza “msamaha wa dhambi” kuwa “ruhusa ya kutenda dhambi”. Alifanya kazi maisha yake yote kufichua mafundisho haya ya uongo na uongo wa Shetani, katika maandishi yake na katika mahubiri yake. Kazi ya utume ya mtu huyu mnyenyekevu imewasaidia watu wengi kuwa wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo, na kuingia katika maisha na ushirika wa kina zaidi pamoja Naye.
Sigurd Bratlie aliandika mamia ya makala na vitabu vingi kuhusu maisha ya Kikristo na ufahamu wa Maandiko. Nukuu zifuatazo zimetokana na baadhi ya vitabu vyake. Maandiko haya yanaweza kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha yako ya Kikristo mwenyewe.
Neema
“Haitufariji kusikia kwamba neema ni kuu kiasi kwamba hata tukifungwa na dhambi, bado tutafika mbinguni. Faraja yetu ni kwamba neema ya Mungu ni kuu kiasi kwamba hatuhitaji tena kufungwa na dhambi; sasa tunaweza kuishinda dhambi. Hiyo ndiyo mbingu kwetu!”
Damu ya Yesu
“Damu ya Yesu ni zaidi ya damu ya mbuzi na mafahali. Kupitia damu Yake tunapokea si msamaha tu wa dhambi zetu bali pia tunawekwa huru, kiasi kwamba hatuhitaji tena kuendelea kutenda dhambi zilezile tena na tena. Damu ya mafahali na mbuzi ingeweza tu kutakasa mwili (asili yetu ya dhambi) kutokana na dhambi ambazo tayari zilikuwa zimefanywa. Lakini damu ya Kristo inaweza kuitakasa dhamiri yetu kutokana na matendo yaliyokufa, ili tuweze kumtumikia Mungu aliye hai! (Waebrania 9:14.) Kwa maneno mengine, hatuhitaji tena kuwa watumwa wa dhambi.”
Ukamilifu
“Tunapozungumza kuhusu kuwa wakamilifu, tunamaanisha kuwa wakamilifu katika dhamiri yetu kama wanafunzi—na hili linawezekana! Kuanzia hapo, tunapaswa kuendelea kukamilishwa (kuwa zaidi kama Yesu). Yesu anasema, ‘Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake…’ Mathayo 10:25. Lakini hadi tuwe hivyo, lazima tuwe maskini wa roho, na tuwe na njaa na kiu ya ukamilifu huu.”
Neema ya kweli ni kuu sana
“Neema haimaanishi msamaha tu, pia inamaanisha msaada (Waebrania 4:16). Neema haitolewi tu ili kutusamehe dhambi zetu, bali pia kutufundisha tusiendelee kutenda dhambi (Tito 2:11-12).”
Kupotosha maneno ya Yesu
“Watu wengi wanapopewa maonyo, husema, ‘Hatuwezi kufanya chochote.’ Wanamnukuu Yesu, jambo linalowafanya wahisi kuwa wako sawa. Lakini wanayapotosha maneno Yake, kama vile watu wengi wanavyopotosha neno la Mungu kwa kulifanya liwafae wao wenyewe. Yesu alisema nini kweli? “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, kwa maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lolote.” Yohana 15:5. Basi wanaposema, ‘Hatuwezi kufanya chochote,’ kwa kweli wanakuwa wanasema kwamba wako nje yake. Hilo linamaanisha kwamba wao si wanafunzi Wake na pia si viungo vya mwili wa Kristo.”
Hila za Shetani
“Tunaona jinsi watu wanavyogeuka kwa urahisi kutoka kwa Mungu katika mioyo yao. Shetani anachohitaji ni kuwapa mpenzi wa kiume au wa kike, pesa zaidi au sifa kutoka kwa watu. Mara nyingi anahitaji tu kugusa mali zao au kuwaruhusu watendewe isivyo haki, au kuruhusu jambo fulani litokee wasilolielewa. Wengi wamegeuka mbali na Mungu katika mioyo yao. Imani yao imeshindwa, na Shetani amefurahi. Ikiwa umeshindwa na ukaanguka, kumbuka - kama ungalielewa tu kilichokuwa muhimu kweli, mgogoro ulikuwa kuhusu nini, basi ungalifurahi katika majaribu yako.”
Jaribu—sababu ya kufurahi
“Watu wengi hufikiri kwamba kujaribiwa ni sawa na kutenda dhambi; lakini kama hilo lingekuwa kweli, Yakobo angewezaje kutuambia tufurahi (Yakobo 1:2)? Kinyume chake, wale wanaoamini ushindi juu ya dhambi hushinda taji la uzima katika majaribu [majaribu ya kujaribiwa], kama tunavyosoma katika Yakobo 1:12: ‘Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.’”
Neno ni Neno la Mungu
“Jiwekeni mbali na maneno yote mepesi na matupu na porojo! Msibishane na watu kuhusu Neno la Mungu. Lipokeeni kama Neno la Mungu, na mliamini kama lilivyoandikwa. Ndipo litafanya kazi kwa nguvu ndani yenu. (Tazama 1 Wathesalonike 2:13.)”
Msaada wa kufanya mapenzi ya Mungu
“Mwili pamoja na tamaa zake za dhambi hutuzuia kufanya mapenzi ya Mungu. Tamaa hizo ni kubwa mno kwetu na hutufanya tutende dhambi, hata kama kwa kweli tunataka kufanya mapenzi ya Mungu. Ndiyo maana Mungu alimtuma Mwana Wake na akatupatia injili—habari njema. Habari njema ni hii: ‘Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.’ Wagalatia 5:16. Hivi ndivyo Yesu alivyotufanyia iwezekane alipokuwa Mwana wa Adamu.”
Agano jipya
“Ikiwa mmefanya uamuzi thabiti wa kutii mapenzi yote ya Mungu, basi Bwana anaahidi kuwapa nguvu kutoka juu, kuwapa kila kitu mnachohitaji kwa ajili ya maisha ya utauwa, kuziandika sheria Zake katika mioyo yenu na akili zenu, na kuwabariki kwa baraka zote za kiroho. Kila kitu mnachohitaji kwa maisha yenu ya kila siku pia mtapewa. Ni nini kingine ambacho mngetamani?”
Umuhimu mkubwa wa maisha ya Yesu kwetu
“Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu, ilithibitisha kwamba hakuwahi kutenda dhambi, ingawa alikuwa na asili hii ya kibinadamu ambayo tunajua ndani yake hamna kitu chema. (Tazama Warumi 7:18.) Alimrudia Baba, akiwa hajachafuliwa na mwili wa Daudi. Hii ina maana kwamba, kupitia injili, sisi pia tunaweza kushinda dhambi na kuja kwenye maisha yale yale aliyoyaishi Yeye.”
Kufinyangwa ili tufanane na Kristo
“Yesu ni jiwe kuu la pembeni. Ni kwa kutimiza mapenzi ya Mungu kwamba Alifanywa kuwa jiwe kuu la pembeni. Alipokuja ulimwenguni Alisema, ‘Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.’ Waebrania 10:7. Tunaingia katika agano jipya kwa njia ileile kabisa. Sasa pia ni kwa kutimiza mapenzi ya Mungu kwamba tunafanywa kuwa kama Yeye. Katika Maandiko imeandikwa kuhusu sisi.”
Maisha yetu hayawezi kufichwa
“Uzima ni nuru ya wanadamu; hakuna mtu anayeweza kukopa nuru kutoka kwa mwingine. Pia leo, wapo watu wanaoishi katika dhambi lakini wanajaribu kujificha miongoni mwa Wakristo. Wengine wanawaamini kwa sababu wanahudhuria mikutano ya kanisa, na wanaonekana kuwa watu wema. Lakini wakati utakuja watakapofichuliwa kuwa walivyo hasa.”
Maana halisi ya kushinda
“Kuna ahadi kubwa kwa wale wanaoshinda (Ufunuo 2 & 3). Kushinda maana yake ni kwamba hufanyi matendo mema ili watu wakusifu, bali unafanya kila kitu kwa ajili ya Yesu kwa sababu unampenda. Ukifanya hivi, wewe ni mwenye hekima kweli. Kisha utanyakuliwa Yesu atakaporudi kuwachukua wale walio tayari. Utawekwa katika mavazi meupe na utaweza kutembea pamoja na Yesu, naye ataikiri jina lako mbele ya Baba na malaika wake (Ufunuo 3:5).”