Siku zote ilikuwa vigumu sana kwangu kukubali kukosolewa kuhusu jambo Fulani nililofanya kwa nia njema. Kusema kweli ilikuwa moja ya udhaifu wangu mkubwa. Kila niliposhutumiwa kuhusu jambo Fulani, nilipambana na mawazo mengi ya giza na kuvunjika moyo. Ningehisi kwamba sikuwa mwema vya kutosha. Ningehisi kwamba sikueleweka na ningekuwa na shaka ikiwa kweli nilikuwa na uwezo wa kutenda mema.
Baada ya haya kutokea mara kadhaa, nilianza kujiuliza sana nini chanzo cha tatizo. Kwa nini mambo hayakuwa mazuri wakati nilikuwa na uhakika kwamba nilikuwa nimetii kwa uaminifu mambo ambayo Mungu alikuwa amefanya ndani yangu?
Kisha siku moja mistari hii ilikuja akilini mwangu; “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani ndani ya mwili wangu , halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.” Warumi 7:18. “Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.” Warumi 3:10-12.
Niliposoma mistari hii, ilidhiirika kwamba nina dhambi katika asili yangu ambayo huathiri mema yote ninayojaribu kutenda. Matokeo yake, nia yangu ya kibinafsi huja wakati wowote ninapojaribu kufanya jambo jema. Naona licha ya kutaka kutenda mema pia napenda kusifiwa na kushukuriwa na nina mategemeo ya namna ninavyopaswa kutendewa na kadhalika. Lakini je, hilo linamaanisha kwamba niache kujaribu kutenda lililo jema? Hivyo pia isingekuwa sawa.
Suluhisho lilikuja nilipogundua kwamba nilipaswa kwanza kukubali ukweli – kwamba hakuna neno jema katika asili yangu ya kibinadamu. Kisha ilinibidi kuwa na imani katika ahadi za Mungu ambazo zimeandikwa kotekote katika Biblia. Ilinibidi kuanza kuamini kwamba Mungu anaweza kunisafisha kutoka kwenye dhambi na kunibadilisha kuwa kama Yesu, hatua kwa hatua kila siku kama ilivyoandikwa katika Warumi 8:29.
Imani katika ahadi za Mungu ikawa rafiki yangu wa karibu
Imani katika ahadi za Mungu ikawa rafiki yangu wa karibu sana, na nikashikilia mstari huu; “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.” Wafilipi 1:6.
Kadri nilivyosoma neno la Mungu, ndivyo mistari na ahadi nyingi zilinibidi kuzishikilia. Kwa mfano, kulikuwa na Wakolosai 3:23-24: “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu. Mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.”
Kurudi nyuma ninapokosolewa au kupokea maoni hasi ni jambo la zamani, kwa sababu sikubali tena kile ninachohisi. Ninachagua kuukubali ukweli na kupigana kushinda mawazo mabaya, hisia na vishawishi vinavyoniijia katika hali hizi badala ya kujinyenyekeza. Ninapofanya hivi, Mungu anaweza kufanya kazi nami na kunibadilisha. Kila siku, katika hali zote ninaweza kupata hasira, kiburi na dhambi nyingine iliyo ndani yangu, nikubali na baada ya muda, ninaweza kuwa mmtu mpya kabisa aliyejazwa na matunda ya roho. Ni muujiza kiasi gani!
Kamwe usikatishwe tamaa
Ushuhuda wangu ni kwamba sikumbuki ni lini mara ya mwisho nilivunjika moyo. Haiwezekani nikatishwe tamaa nikiamini ahadi za Mungu! Kisha niko huru kutokana na hali duni, nikijilinganisha na wengine, wivu, kuhisi tuhuma, n,k. Shetani anayetaka kunishtaki kila wakati (Ufunuo12:10), hana budi kunikimbia, kwa sababu hana nguvu juu yangu. Ninapokiri ukweli na kumshukuru na kumsifu Mungu kwamba atanibadilisha, kidogokidogo. Pia ninashikilia wazo kwamba baada ya muda, “kidogokidogo” itakuwa ya kutosha!
“Kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; Mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu Pamoja na furaha.” Wakolosai 1:10-11.
Namshukuru Mungu kwamba inawezekana kuwa huru kutoka kwenye kuvunjika moyo na hisia za kutokuwa mwema vya kutosha. Namshukuru yeye kwamba ninaweza kuona kile anachotaka kunionesha kuhusu mimi mwenyewe kila siku na kwamba ninaweza kuwa na furaha kwamba naweza kubadilika na kuwa kama Yesu.