Watatu waliosulubiwa na wafuasi wao.

Watatu waliosulubiwa na wafuasi wao.

Wanaume watatu walisulubiwa Kalivari, lakini siku iliisha kwa matokeo matatu tofauti. Mfano wako ni nani?

31/3/20183 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Watatu waliosulubiwa na wafuasi wao.

“Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la kichwa, ndipo walipomsulubisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume na mmoja upande wa kushoto. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Kisha akasema, ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, amini, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi” Luka 23:33, 39-43.

Yesu aliwekwa kwenye msalaba wa kati, mwana wa Mungu. Kwa hiari yake mwenyewe alikuja duniani katika mwili kama wetu na asili ya kibinadamu ambayo ilikuwa na tabia ya dhambi na tamaa kama sisi. Alikua na mapenzi ya kibinadamu kama yetu lakini kamwe hakufanya mapenzi yake, kila mara aliyakataa na kufanya mapenzi ya baba, na kwa njia hii hakutenda dhambi kamwe. Alitupenda sana alitaka kumwokoa kila mtu, lakini watu hawakuupenda ukweli aliotakiwa kuwaambia. Hapo walimtundika mtu asiye na hatia ambaye hakutenda dhambi kamwe na alifanya mapenzi ya baba yake pekee kuanzia siku aliyokuwa mkubwa vya kutosha kuelewa.

Katika misalaba mingine miwili walitundikwa wahalifu, watu ambao mara nyingi walifanya mapenzi yao na kamwe hawakuwahi kufanya mapenzi ya Mungu. Wote waliishi dhambini. Lakini kulikua na tofauti kuu na muhimu sana kati ya hawa wahalifu. Mmoja alikuwa mgumu na asiyeamini, wakati mwingine alikua na moyo laini, alikua wazi kusikia ukweli na kuamini. Mmoja hakuhisi aibu wala kujutia matendo yake na hiyo alibaki nje, wakati mwingine aliingia paradiso pamoja na Yesu.

 

Hakuna mmoja kati ya hawa watu wawili aliyemfuata Yesu katika hatua zake (1Petro 2:21) katika maisha yao, na sasa hawakuwa na muda zaidi ya kufanya hivyo. Hivi ndivyo ilivyo kwa kila mtenda dhambi ambaye amebadilishwa tu katika muda wake wa mwisho wa maisha.

Sote tunapaswa kuanza kama mhalifu mmoja, kwa maombi ya haraka kwa ajili ya rehema na msamaha wa dhambi zetu. Sote tunapaswa kuanza kama “wahalifu”. Lakini kwa kuwa mhalifu huyu ni mfano wa namna ya kuanza katika njia ya ukombozi, ambayo haimanishi kwamba ni mfano wetu tunapoendelea. Wengi wameitwa na kupewa fursa kumfuata yeye aliyesulubiwa katika msalaba wa katikati na kutembea katika nyayo alizoziacha - ambaye kamwe hakufanya mapenzi yake lakini akishinda dhambi zote ambazo ziliishi ndani ya asili yake ya kibinadamu wakati wa maisha yake duniani.

Ukweli ni kwamba watu wote, kwa kujua ama kutojua wanaingia katika makundi haya matatu na kufuata mmoja kati ya hawa watatu waliosulubiwa.  Wale ambao kwa neema ya Mungu, wanashinda dhambi wanamilikiwa na kundi la kati. Wale ambao hawashindi lakini hukiri dhambi zao na kuomba msamaha wanamilikiwa na kundi la pili; wale ambao hawatubu na hawaombi msamaha wanamilikiwa na kundi la tatu.

Kwa bahati mbaya, waumini wengi humtazama mhalifu aliyetubu kama mfano wao na kupata Faraja kwake; hujifariji wenyewe kwa maombi ya mtoza ushuru kwa sababu ileile (Luka 18:13). Ni kweli kabisa kwamba tunapaswa kuanza kama hivi. Lakini si kweli, kama wengi wanavyofikiri, kwamba tunapaswa kuendelea kama hivi mpaka mwisho.

Chapisho hili linapatikana katika

Makala hii imetafsiriwa kutoka kinorwe na awali ilichapishwa mwaka 1973 kama sura katika kijitabu “Nimesulubiwa pamoja na Kristo” cha Elias Aslaksen. Imechukuliwa na kupewa ruhusa kutumika kwenye tovuti hii.