Biblia inasema nini kuhusu Mpinga Kristo?

Biblia inasema nini kuhusu Mpinga Kristo?

Ufafanuzi juu ya mada ya kupendeza ambayo mara nyingi hueleweka vibaya.

28/10/20166 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Biblia inasema nini kuhusu Mpinga Kristo?

Kuhusu Mpinga Kristo

Mpinga Kristo ni kinyume cha Kristo. Kama vile Kristo alikuja duniani kufanya mapenzi ya Mungu, Mpinga Kristo atakuja kufanya mapenzi ya Shetani. Atakuwa Shetani katika umbo la mwanadamu.

 

Lengo lote la Shetani ni kuwa kama Mungu kwa nguvu na uweza, na anaifanyia  kazi kwa nguvu zake zote, usiku na mchana. “Yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho mungu ama kuabudiwa; hata yeye  mwenyewe huketi katika hekalu la Mungu, akijionesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” 2 Wathesalonike 2: 4 . Lengo lake ni kuchukua nafasi ya Mungu, na atamtuma Mpinga Kristo kama njia ya kutekeleza hilo. Mpinga Kristo atakataa kwamba watu wanahitaji Mungu, na atajionesha kama mtawala wa ulimwengu huu.

 

Lakini ni ulimwengu gani utamkubali  wakala wa shetani kama bwana?  Je, Inawezekanaje kuwa ulimwengu huu tuishio umefika katika hali hii?

Roho ya Mpinga Kristo

Roho ya kawaida ulimwenguni ni roho ya Mpinga Kristo, ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu siku za mwanzo za kanisa. (1 Yohana 4). Roho ya Mpinga Kristo inaweza kuelezwa kama kila roho isiyokiri kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili (1 Yohana 4: 2). Inadai kwamba Yesu hakuwa na tamaa kama mtu wa asili, na kwa hivyo, hakuweza kutenda dhambi. Lakini katika neno la Mungu imeandikwa kwamba alikua na mwili na damu kama sisi.

“Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za  mauti, yaani ibilisi”. Waebrania 2:14.

Alikuwa na tamaa zile zile, ambazo zilimfanya ajaribiwe, na ilimbidi apigane ili asitende dhambi. Alikuwa na Roho Mtakatifu wa kumwongoza, na nguvu na msaada kutoka kwa Baba yake aliye mbinguni. Alifanya hali hii ipatikane kwetu, na kwa hivyo tuna uwezo wa kumfuata kwa njia ambayo aliifungua kupitia mwili na kurudi kwa Baba. Ebr. 10:20.

 

Hiyo inamaanisha tunapaswa kuweka juhudi sawa, kupigana vita vile vile alivyofanya, kupigana dhidi ya dhambi ambayo tunayo katika asili yetu ya kibinadamu (katika mwili wetu) kama matokeo ya anguko la Bustani ya Edeni. Watu wengi hawako tayari kufanya hivyo. Na ndivyo roho ya Mpinga Kristo inavyopata nguvu. Inaonesha watu njia rahisi.

Soma pia: Roho ya Mpinga Kristo: inakana kwamba Yesu alikuja katika mwili

Kutengwa kwa Mungu na watu

Dhambi ndiyo sababu tunatenganishwa na Mungu. Dhambi inapofutwa, tunakua kitu kimoja na Mungu. Roho ya Mpinga Kristo inaruhusu dhambi kuishi kwa kuwafunika kwa uvumilivu, "upendo", na uhuru. Neno la Mungu linasema wazi ni nini kilicho sawa na  ni nini  kilicho kibaya, ni nini kilicho dhambi na ni nini kilicho  safi. Lakini wakati watu wengi  wanaishi katika dhambi, kwa mfano uzinzi, hawaioni tena kama dhambi. Sheria za Mungu zinakataliwa, na sheria za jamii, na baadaye hata sheria za mataifa, hubadilika.

Kwa hivyo uchafu na dhambi zinaruhusiwa kuishi, na watu huenda mbali zaidi na Mungu - ambayo ndivyo Shetani anataka. Walimwengu wengi husikiliza roho hii, kwa sababu inawaruhusu kuishi kwa raha, bila dhamiri yenye hatia. Hapo zamani, hii ilifanywa chini ya mwavuli wa dini na msamaha wa dhambi bila kuachana  na  dhambi. Lakini katika nyakati tunazoishi sasa, ubinadamu unazidi kuchukua jukumu ambalo dini ilikuwa ikifanya. Watu hujitegemea zaidi na zaidi, badala ya kuongozwa na "nguvu yoyote ya juu".

Soma pia: Dhambi ni nini?

Ufunuo wa Mpinga Kristo

Yote haya ni kuandaa njia ya Mpinga Kristo mwenyewe kuja na kuondoa aina yoyote ya dini. Atasema kwamba Mungu hahitajiki hata kidogo. Atafanya ishara na maajabu kuthibitishia ulimwengu kwamba  watu wanaweza kujitunza na hawahitaji Mungu. (Ufunuo 13: 13-14.)

Watu wako tayari kumkubali mtu kama huyo. Mtu asiyezuia maisha yao ya starehe - ambaye atawapa amani na maelewano hapa duniani; ulimwengu wa uvumilivu na upendo, bila gharama yoyote ya kibinafsi kwao. Na Mpinga Kristo ataweza kufanya hivyo.

Jina la Mpinga Kristo limekuwa likiunganishwa na uovu kila wakati, lakini ukweli ni kwamba wakati atakapofunuliwa, watu wengi hawatamtambua kama Mpinga Kristo. Hataonekana mwovu; kinyume chake, atakuwa mtu ambaye ana talanta, anayetaka kutatua matatizo ya ulimwengu. Atafanya kazi kuufanya  ulimwengu kuwa paradiso, bila Mungu (kitu ambacho tayari kimeanza kutokea). Ulimwengu utaamini kuwa Mpinga Kristo akiwa kwenye amri, watu wanaweza kufanya chochote.

“Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni”. Ufunuo 13:6

Wakati hilo likitokea, mwishowe Shetani atapata alichokuwa akitaka kila wakati. Ataonekana kuwa sawa na Mungu. Atakuwa na udhibiti wa ulimwengu ambao hauna haja ya Mungu.

Bibi-arusi wa Kristo

Lakini kuna wengine ambao hawajakataa na hawatakataa injili ya Kristo; wanataka kumalizana na dhambi ambayo wanaiona ndani yao, ili waweze kuwa kitu kimoja na Mungu. Hawatadanganyika, kwa sababu kwao dhambi ni dhambi. (Warumi 7:13.) Kwa sababu wamekuwa macho sana na kuwa makini sana kwa roho yoyote inayostahimili dhambi, watamwona Mpinga Kristo kwa jinsi alivyo.

Wakati hili linatokea, wanaweza kutarajia kurudi kwa kristo na kumchukua bibi-arusi wake kwenda nyumbani kuwa naye. Mara tu wanaponyakuliwa na kupokea tuzo la uaminifu wao, Mpinga Kristo anaweza kufanya anachokitaka. (2 Wathesalonike 2: 6-7.) Huu utakuwa wakati mbaya duniani. Hali ya kweli, mbaya ya Mpinga Kristo itafunuliwa. Wakati mambo yamekuwa mabaya kama inavyoweza kuwa, wakati uhitaji ni mkubwa, Kristo atarudi tena na bibi-arusi wake.

Halafu atamwua Mpinga Kristo kwa pumzi ya kinywa chake, na ulimwengu utaona jinsi Mpinga Kristo alivyo dhaifu. Yesu atasimamia falme za dunia, Shetani atafungwa na kutupwa ndani ya shimo lisilo na mwisho, na dunia itakuwa na miaka elfu ya kujifunza jinsi mapenzi makamilifu ya Mungu yanavyofaa, yenye haki, ya kweli, na mema, yaliyo uhuru bila udanganyifu wa shetani. Na wale waliojiweka safi kutoka kwa roho ya Mpinga Kristo na wamemfuata Yesu kwa uaminifu wao mpendwa, wataishi na kutawala na Kristo katika Milenia hii. (Ufunuo 20). Ufalme wao wa mbinguni utakuwa wa milele!

Chapisho hili linapatikana katika

Makala hii ilichapishwa hapo awali kwenye https://activechristianity.org/ na imebadilishwa na ruhusa ya matumizi kwenye wavuti hii.