Je, umeridhika?

Je, umeridhika?

Hebu fikiria ikiwa unaweza kusema mwishoni mwa maisha yako: "Hiyo ilikuwa bora zaidi kuliko nilivyofikiria ingekuwa!"

30/1/20244 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Je, umeridhika?

5 dak

Je, umewahi kuwa na lengo maishani mwako, na ulipolifikia, ukajiambia, “Sina hakika kwamba hilo lilifaa,” au pengine, “Sivyo nilivyofikiri lingekuwa”?

Kwa upande mwingine, je, uliwahi kuchagua kufanya jambo fulani na baadaye ukafikiri, “Nilifikiri hili lingekuwa zuri, lakini ni bora zaidi kuliko vile nilivyofikiria kuwa lingekuwa”? Fikiria jinsi ingekuwa ya kuridhisha na nzuri ikiwa umetoa maisha yako yote kwa kitu na kufikiria hivyo baadaye! Watu ambao wamejitoa wenyewe kwa moyo wote kuwa wanafunzi wa Yesu wanaweza kusema hivi mwisho wa maisha yao.

Baada ya Paulo kukutana na Yesu njiani kuelekea Damasko, alisema: “Bwana wataka nifanye nini?” Matendo ya mitume 9:3-6. Baadaye alitoa ushuhuda huu kuhusu maisha aliyoyachagua: “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu…” Waefeso 3:20

Petro alikuwa mmoja wa wavuvi wanne ambao “mara moja waliacha nyavu zao” ( Marko 1:16-20 ) Yesu alipowaita, na anaandika hivi: “kwa kuwa uweza wake na uungu umetukrimia vitu vyote vipasavyo uzima na utaua, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo umetukrimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.” 2 Petro 1:3-4.

Yuda anasema yafuatayo mwishoni mwa barua yake: “Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu…” Yuda 1:24-25.

Hawa na wengine wengi ambao waliacha kabisa kile ambacho wangeweza kuwa katika ulimwengu huu ili kumfuata Yesu, hawakujutia uchaguzi ambao walifanya.

Watu wengi wanataka maisha marefu na yenye furaha kama haya, lakini hawayaoni. Katika Isaya 55:1-2 Mungu anatuambia jinsi ya kupata uzima huu: “Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, naye asiye na fedha njoi, nunueni mle Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, bila fedha na bila thamani. Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidi, mle kilicho chema, na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono.”

.Sura inaendelea kututia moyo tumtafute Bwana na kusikiliza neno Lake. “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula, ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma. Maana mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani…” Isaya 55:10-12.

Yesu alimwambia mwanamke Msamaria aliyekutana naye kisimani hivi: “Kila anywaye maji haya ataona kiu tena walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya yakibubujikia uzima wa milele.” Yohana 4:13-14. Hili, tunaweza kusema, ni utimizo wa yale ambayo Isaya alisema kuhusu Yesu: “… Naye atakamilisha mambo ambayo BWANA anataka afanye. Baada ya nafsi yake kuteswa na mambo mengi, atayaona maisha na kuridhika.” Isaya 53:10-11.

Vivyo hivyo, Yesu atamridhisha mtu yeyote ambaye atafuata hatua zake: “Kusudi langu ni kuwapa maisha yenye kuridhisha na uzima tele.” Yohana 10:10 . Tukichagua kuwa wanafunzi Wake, tutakuwa na maisha yenye baraka tukiwa duniani na hata umilele wenye furaha zaidi baadaye.

Kwa mifano na ahadi kama hizo tulizopewa, je, si jambo la hekima “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu”? Isaya 55:6.

Chapisho hili linapatikana katika

Makala haya yanatokana na makala ya Steve Lenk yaliyochapishwa awali kwenye https://activechristianity.org/ na yamebadilishwa kwa ruhusa ya matumizi kwenye tovuti hii.