“Mwendee mchwa, ewe mvivu; zitafakari njia zake, ukapate hekima.” Mithali 6:6.
Uwe mwenye bidii
Mchwa hujenga kichuguu chao kwa njia bora iwezekanayo ili kubaki na joto. Mara tu jua linapochomoza, mchwa huanza kufanya kazi. Njia zote za mchwa huishia kichuguuni; kila mchwa hufanya kazi kadiri awezavyo. Fimbo ikimzidi mchwa mmoja, wengine watakuja na kusaidia kuipeleka kichuguuni.
Uvivu huleta ulegevu, na ulegevu huleta upungufu. Angalia jinsi mchwa wanavyofanya kazi. Kwanza ya kawaida, kisha ya rohoni. “Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.” Mithali 6:7-8.
Fanya kazi kwa bidii
Ni baraka kufanya kazi kwa mikono yako na kufanya kazi katika roho. Kuna chakula kingi katika nchi zisizolimwa za maskini. Wanawali wapumbavu waliwaomba wanawali wenye hekima mafuta. Huo ndio mwisho wa wale walio wavivu. Hufikia kuombaomba. Wanawali wapumbavu hawakukusanya mafuta katika vyombo vyao. Walikuwa wavivu. Inahitaji juhudi kukusanya chakula, kwa mtazamo wa kawaida, na juhudi kama hizo hizo zinahitajika kukusanya chakula cha rohoni. Kwa mtu mvivu, kazi huhisiwa kama adui mwenye nguvu; huhisi kama laana ambayo haiwezekani kushinda—na hiyo ni mtazamo wa kutisha!
Katika mikutano yetu, pia kuna watu ambao, kwa mtazamo wa rohoni, hawana chochote cha kutoa kamwe. Wanataka tu kupokea. Wanafumbua midomo yao tu kama vifaranga, wakitarajia wengine wawalishe. Hili ni la kawaida mwanzoni mtu anapokuwa bado mtoto wa rohoni; lakini ikiwa hali hiyo bado ipo wakati ambao mtu anapaswa kuwa na uwezo wa kuwafundisha wengine, si sawa.
Kichuguu na hekalu
Kanisani, njia zote pia huelekea kwenye “kichuguu”—yaani, kwenye hekalu la kiroho linalojengwa; kwa maana tunajengwa pamoja na wengine kuwa maskani ya Mungu kwa Roho (Waefeso 2:22). Mambo yote na yafanywe kwa ajili ya kujenga. Uwe mwenye bidii katika kuujenga ufalme wa Mungu. Ikiwa “fimbo” ni nzito mno kwa ndugu yako, basi nenda ukamsaidie kuibeba. Sio wote ni wahudumu wa Neno, lakini kila mtu anaweza kuwa mtumishi wa Mungu hekalu linapopaswa kujengwa. Hatuna mtawala, afisa wala mkuu, kama vile mchwa wasivyo nao, na bado kazi hufanyika kwa haraka. Wote hujenga kulingana na msukumo na nia ya ndani. Ndivyo inavyopaswa kuwa.
“Utalala hata lini, ewe mvivu? Utaamka lini kutoka usingizini mwako? Kulala kidogo, kusinzia kidogo, kukunja mikono kidogo upate kupumzika; umaskini utakujilia kama mnyangʼanyi, na uhitaji kama mtu mwenye silaha.” Mithali 6:9-11.