Alihesabiwa haki kwa sababu ya imani
Watu wengi ambao huzungumza kuhusu haki tunayohesabiwa hufikiri juu ya watenda dhambi wanaoamini upatanisho, hivyo maisha ya Yesu—haki yake—inahesabiwa kuwa haki yao, ingawa hawastahili. Watu wachache ndio wanaofikiri kwamba haki ya Yesu inapaswa kuwa maisha yao ya kibinafsi; watu wengi hufikiri ni jambo ambalo wanahesabiwa tu.
Hali haikuwa hivyo kwa Ibrahimu. “Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.” Mwanzo 15:6. Mungu alikuwa amemuahidi mtoto wa kiume. Ibrahimu angalikuwa ametenda dhambi kubwa ya udhalimu kama asingaliamini - angalimfanya Mungu kuwa mwongo. Lakini Ibrahimu alimpa Mungu utukufu na akaamini kwamba Mungu angetenda kile alichoahidi. Ukweli kwamba aliamini, hilo lilihesabiwa kwake kuwa haki. Kwa maneno mengine, alikuwa mwenye haki kwa sababu aliiamini ahadi. Aliamini kwamba Mungu angempa mtoto wa kiume. Ingawa alikuwa mzee na tumbo la Sara lilikuwa limekufa, hakutilia shaka bali alizidi kuwa hodari katika imani alipompa Mungu utukufu (Warumi 4:19–24). Ukweli kwamba Ibrahimu alimpa Mungu utukufu wote lilithibitisha haki yake.
Ahadi
Hili liliandikwa kwa ajili yetu. Ni nani anayeamini kwamba Mungu ni mwaminifu na atatimiza ahadi zake? Mungu pia ametupa sisi, ambao ni watu wenye dhambi, ahadi kuu. “Ambazo kwa hizo ametukirimia ahadi kuu mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu …” 2 Petro 1:3–4. Mtu anayeamini kwamba hili litatokea kwake anaamini kwamba Mungu ni mkweli na mwaminifu, na hilo litahesabiwa kwake kuwa haki.
“Na ninyi ... amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama.” Wakolosai 1:21-22
Hizi ni ahadi za utukufu, lakini ni nani anayeziamini ili ahesabiwe kuwa haki kwake? Waumini wengi wamepoteza imani kwamba Mungu ni mwaminifu na wa kweli. Hawamini kwamba atawatendea hivyo, na kwamba anaweza kufanya hivyo ingawa wao ni watenda dhambi wakuu. Hapana, hawaamini kwamba Mungu anaweza kufanya hivyo, kwamba anaweza kufanya kazi hiyo pamoja nao.
Basi wanaamini kwamba yeye atahesabu haki ya Yesu kwao tu, bila ahadi zozote kutimizwa katika maisha yao wenyewe. Wanadhani inapaswa tu kuhesabiwa kana kwamba ndivyo ilivyo. Je, hilo linampa Mungu utukufu? Je, ni haki kuamini kwamba Mungu huzitendea ahadi zake hivyo? Je, unaamini kwamba imani hii itahesabiwa kwako kuwa haki? Maelfu ya watu wanaishi katika neema hii ya uongo ambayo Yuda anaandika kuihusu katika Yuda 4, na Mungu hawezi kutimiza ahadi zake katika maisha yao.
Haki—si tu kuhesabiwa kuwa hivyo, bali kuwa uhalisia
“Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.” Warumi 8:25.
Mtu ambaye hasubiri kwa hamu hilo naye haamini pia. Ibrahimu aliamini, naye alisubiri kwa hamu Isaka azaliwe—kutimizwa kwa ahadi. Alipokea kile alichoamini—alimpokea Isaka. Ibrahimu aliacha nyayo za imani nyuma yake (Warumi 4:12)! Aliitii Mungu alipomwita (Waebrania 11:8).
Sisi ni watoto wa Abrahamu ikiwa tunaishi katika utii wa imani. Ndipo tupokeapo kile ambacho Mungu ameahidi (Wagalatia 3:7)— tunashiriki katika hali ya kimungu. Tunasubiri kwa hamu hiyo na kuukimbia uharibifu uliomo ulimwenguni kwa sababu ya tamaa ya dhambi. Tunafanya kila jambo bila kunung’unika wala kutilia shaka ili tuwe wasio na lawama wala hatia, “… wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,” Wafilipi 2:14–15
Hapa tunaona wazi kwamba ahadi si kitu ambacho tunajifanya tu kuwa ni kweli, ambacho kitahesabiwa tu kwetu. Imekusudiwa itimizwe katika maisha yetu hapa duniani. Na tukimwamini Yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, hilo litahesabiwa kwetu kuwa haki (Waefeso 3:20).