“… mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa,” asema Petro katika 2 Petro 1:4.
Ni nini uharibifu uliomo duniani? Ni nini uharibifu katika nyumba? Ni nini uharibifu kati ya watu waliooana? Ni nini uharibifu katika kanisa? Au ni nini uharibifu katika moyo wako mwenyewe?
Uharibifu huu wote ni kujipenda mwenyewe, nao huenda pamoja na ulafi, kiburi, husuda, umbea, mabishano, na taabu nyingine zote. Ni uharibifu na uharibifu wa haki, wa amani, wa furaha, wa uhusiano mzuri kati ya watu – kati ya watu duniani, kati ya wenzi wa ndoa, kati ya watoto na wazazi wao, kati ya washirika wa kanisa moja, na kati ya waumini kwa ujumla.
Na uharibifu huu wote unatoka wapi? Unatoka katika tamaa ya dhambi!
Petro alisema kwamba kama unataka kuwa mshirika wa asili ya kiungu, unapaswa kuokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa ya dhambi.
Ukihisi kwamba mtu anakutumia vibaya, hilo huamsha kitu ndani yako mara moja. Huwasha cheche ndani yako, huanza kuwaka ndani yako, “na kuutia moto maisha yako yote” kama tunavyosoma katika Yakobo 3:6. Na kabla hujatambua, hupasuka katika maneno unayozungumza. Hivi ndivyo uharibifu unavyoingia ndani ya nyumba. Umewashwa moto na jehanamu, anasema Yakobo.
Kimbia mbali kabisa na uharibifu! Uko karibu sana. Sio kitu kinachotokea tu kati ya wasioamini. Uharibifu upo kila mahali ambapo tamaa za dhambi zinatawala - hata kama ni kidogo sana. Sio tu kati ya wasioamini, bali hata ndani ya moyo wako mwenyewe, katika familia yako, na katika kanisa.
Zima cheche kabla haijawasha moto wa maisha yako. Zuia kabla haijasambaa na kuharibu. Udadisi huleta masengenyo, na ulafi wote huleta husuda. Ukipanda kwa mwili, utavuna uharibifu kutoka kwa mwili. Utavuna uharibifu katika nyumba yako, katika kanisa, na katika moyo wako mwenyewe. Utavuna ulichopanda!
Fikiria uharibifu wote! Uharibifu wote hutoka katika tamaa za dhambi! Mwili pamoja na tamaa zake lazima ufe!
“Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.” Wagalatia 5:24. Hili litaonekana katika maisha yako!