Wokovu katika Yesu Kristo si jambo la haraka na la juu juu. Kazi ambayo Kristo hufanya ndani ya mtu anayempenda kweli ni ya kina na inahusisha kila kitu. Anafika katika sehemu za ndani kabisa na za siri zaidi za moyo wetu, na anahukumu mawazo na nia zetu ili kitu kipya kabisa kiweze kuchipuka hapo. Kazi hii inamaanisha mabadiliko kamili kutoka kwa kila kitu kilichoharibika na kibaya kuelekea kile kilicho safi tu na cha kimungu.
Sote tunaelewa kwamba kazi hiyo tukufu haitokei kwa kutamani tu kuwa mtu bora zaidi. La, inahitaji mapinduzi ya ndani, moyo mpya na uliotakaswa— sio jambo linalotokea mara moja tu, bali mara nyingi katika kipindi chote cha maisha!
Kazi ya Mungu kwa Ayubu
Ingawa Ayubu alikuwa mtu mwenye haki isivyo kawaida, ilibidi atendwe kwa namna maalum ikiwa Mungu angefanya kazi ya milele ndani yake. Majaribu aliyopewa kupitia yalileta unyenyekevu mkubwa ndani yake. Ayubu na rafiki zake walikuwa na mawazo na maoni mengi kuhusu matendo hayo yote, mengi yakiwa ya kweli na yenye kujenga. Hasa Elihu alikuwa na mambo mengi mazuri ya kusema ingawa alikuwa bado kijana sana. Lakini kilichomgusa Ayubu zaidi ni pale Mungu Mwenyewe alipozungumza nae “kutoka katika kisulisuli” moja kwa moja moyoni mwake. Maneno yake yalikuwa na nguvu sana kiasi kwamba kitu fulani kilitokea ndani kabisa ya moyo wa Ayubu, naye hakuwahi kuwa mtu yule yule tena baada ya hapo.
Ujumbe wa Mungu haukuwa mgumu kuelewa. Mungu alimuuliza kuhusu mambo mawili. Alitaka kujua Ayubu alikuwa wapi alipoumba mbingu na dunia, na kama alijua majibu ya baadhi ya mafumbo. (Ayubu 38 na 39.) Ayubu hakuweza kujibu lolote kati ya hayo. Badala ya kusema mengi, Ayubu alianza kujinyenyekeza. Aliweka mkono wake juu ya mdomo wake na akanyamaza.
Kisha Mungu akasema tena na kumwambia juu ya wanyama wawili; kiboko "nilichotengeneza pamoja nawe ... Tazama basi, nguvu zake ... na uwezo wake ..." Na mamba, "Katika shingo yake hukaa nguvu ... Juu yan chi Hapana aliyefanana naye ..." Ayubu 40: 15-16; Ayubu 41:22,33. Wanyama hawa wote wawili wana nguvu nyingi sana; hawasujudu wala hawasalimu amri kwa chochote wala kwa yeyote. Ni wazi kwamba Mungu hakuwa anawafikiria wanyama hao; alikuwa akimfikiria Ayubu. Kwa hiyo, Mungu alihitimisha ujumbe wake kwa Ayubu kwa maneno haya muhimu: "Yeye hutazama kitu kilicho juu; Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi." Ayubu 41:34.
Mabadiliko kupitia unyenyekevu
Maneno haya yalitenda kazi kwa nguvu katika moyo wa Ayubu. Hapo awali, alikuwa amesikia tu habari za Mungu. Sasa alianza kuona, na akaelewa Mungu ni nani na yeye ni nani ikilinganishwa na Mungu. " Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. ... Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu ." Ayubu 42: 2,6.
Ukweli huu ni rahisi sana. Tunajifunza kuhusu haya katika shule ya Jumapili—Mungu ni nani na mimi ni nani. Je, Ayubu hakuelewa hili hapo awali? Bila shaka, kwa namna fulani alielewa. Yeye mwenyewe alisema kwamba alikuwa amesikia habari za mambo haya na kuyafahamu kwa kiasi, lakini ukweli ni kwamba hayakuwa yameingia ndani sana ya moyo wake kiasi cha kubadilisha utu wake wote. Hayakuwa yameleta mapinduzi ya ndani katika maisha yake! Hayakuwa yamebadilisha mtazamo wake juu yake mwenyewe, mke wake, marafiki zake, hali mbalimbali, majaribu, na mambo yote ambayo Mungu kwa wema wake alimletea.
Ilihitaji kunyenyekeshwa sana chini ya mkono mkuu wa Mungu kabla ya sikio lake la ndani kufunguliwa ipasavyo kwa sauti ya Mungu, na akapata nuru kuhusu yeye ni nani hasa. Lakini hilo lilipotokea, Ayubu alikuwa mtu mpya kabisa. Hivyo basi, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa majaribu yote na hali za kutunyenyekesha anazotutumia, kwa sababu wokovu hauwezekani bila hayo.
Siwezi kubadilishwa niwe kama Kristo kwa kubadili tu mwenendo wangu wa nje au kwa kuishi “maisha mazuri ya nje ya Kikristo”. La, ninabadilishwa ninapojinyenyekeza kutoka moyoni chini ya mkono mkuu wa Mungu, kuisikia kweli kuhusu mimi mwenyewe na kuiikubali kutoka moyoni, bila kuipuuza wala kutoa visingizio. Kisha Mungu huandika sheria na amri zake moyoni mwangu kwa kina kiasi kwamba nataka kuzitii kwa moyo wangu wote!
Mabadiliko yote hutokea moyoni! Ndiyo maana Yesu alisema, " safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.." Mathayo 23:26, na: " Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.." Mathayo 15:18.