"Nimechoka sana kuwa na watu wasio na akili, wasio na msaada na wenye hasira kila siku. Sidhani kama naweza kuendelea hivi. Imetosha. Inatokea karibu kila siku, kazini, na marafiki zangu, na nyumbani. Imezidi." Nilijikuta nikifikiria hili tena na tena, na ilianza kuonekana katika miitikio yangu nilipokuwa na watu.
Niliona lazima kitu kibadilike. Hapo ndipo Mungu aliponionyesha njia bora zaidi. Alinionyesha kwamba ninaweza kuchagua jinsi nitakavyoitikia. Ikiwa naweza kuchagua, inamaanisha kuwa suluhisho liko akilini mwangu, katika mawazo yangu. Kupitia Neno Lake, alinionyesha njia ya kuchukua mambo ambayo yalikuwa tofauti kabisa na jinsi nilivyokuwa nikiyafanya hapo awali. Nilifungua Biblia katika Warumi 12:17-21 na kusoma:
“Ikiwa mtu amekukosea, usimlipe kosa. Jaribu kufanya kile ambacho kila mtu anaona kuwa kizuri. Fanya kila uwezalo kwa upande wako kuishi kwa amani na watu wote. Kamwe msilipize kisasi, marafiki zangu, lakini badala yake acha hasira ya Mungu ifanye hivyo. Kwa maana Maandiko Matakatifu yasema, ‘Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipa, asema Bwana.’ Badala yake, kama vile Maandiko yasemavyo: ‘Adui zako wakiwa na njaa, wape chakula; wakiwa na kiu, wanyweshe; kwa maana kwa kufanya hivyo utawafanya waungue kwa aibu.’ Usiruhusu uovu ukushinde; badala yake, shinda [uushinde] ubaya kwa wema.”
Hakuna mahali popote katika aya hizi panaposema, “... isipokuwa watu wanakosa akili au wakorofi.”
Kufanya Neno la Mungu
Kwa hiyo nikaanza kufanya yale ambayo aya hizi zinashauri. Jinsi watu walivyonitendea haikubadilika, lakini sasa nilijua njia bora zaidi ya kuwa pamoja nao. Sio kawaida kwa mtu yeyote kumwambia mfanyakazi mwenzake kuwa na siku njema, na kumaanisha hivyo, baada ya kuwa amekufokea tu! Hakika hili halikuwa jambo ambalo ningefanya kwa kawaida. Lakini Biblia iliniambia niushinde ubaya kwa wema. Si katika asili yangu ya kibinadamu kufanya hivyo, lakini Mungu ni mwema sana hivi kwamba ninaweza kumwendea na kusali ili kupata msaada wa kuitikia kwa njia ya kimungu, haijalishi jinsi watu wanavyonitendea. (Waebrania 4:16.)
Kisha Mungu akanipa mstari mwingine, “Tena tusichoke kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.” Wagalatia 6:9. Huo ndio ulikuwa msaada niliohitaji. Nisipokubali jaribu la kuitikia kwa hasira, ninapanda mbegu nzuri. Siku moja, kwa wakati ufaao, nitavuna. Hebu fikiria, tumeitwa kubariki na sio kulaani! Nimeona kwamba ninapolipa ubaya kwa wema, siku zangu ni bora zaidi. Watu wanaweza kusema au kufanya chochote wanachotaka, lakini hilo haliwezi kuondoa furaha moyoni mwangu.
Kila jaribu ni fursa ya kushinda
Ingawa huenda watu bado wakawa wakorofi, sikubali tena kushawishiwa kuwa na chuki au kukosa subira. Ninaamini yale yaliyoandikwa katika Neno la Mungu, kwa hivyo siruhusu nishindwe na hasira au chuki ninakojaribiwa. Kwa maneno mengine, ninafanya Neno la Mungu. Na nina ahadi kwamba nitavuna vitu vizuri ikiwa nitaendelea kufanya hivi.
“Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu ... Neno la Kristo na liwe ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” Wakolosai 3:15-16. Hiki ndicho ninachotaka kufanya zaidi ya kitu kingine chochote. Hili ndilo ninalojishughulisha nalo, na ninajua kwamba Mungu ataendelea kunisaidia kwa hili, haijalishi ni nani ninayekutana naye, awe mkorofi au la.