Kama wakristo, tunajua kwamba hatupaswi kuogopa kifo. Biblia inaeleza kitakachotokea kwa waliokufa. “Parapanda italia na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, na sisi tutabadilika. Maana mwili huu uharibikao uvae kutoharibika….mauti imemezwa kwa kushinda….. U wapi, ewe mauti, uchungu wako?” 1Wakorintho 15:52-57. 1Wathesalonike 4:16-18 pia ina ahadi tukufu ambayo wale kati yetu wanaomwamini Yesu wanaweza kuitarajia.
Lakini wakati mwingine huwa nashangaa jinsi gani ningekutana na kifo muda wangu wa kufa ulipofika. Naweza sema mambo sahihi na kujua vifungu katika Biblia lakini je, ninaendana na vile nizungumzavyo?
Uzoefu wa kifo
Kwa kupitia uzoefu Fulani niliowahi kuwa nao maishani mwangu ni wazi kwangu kwamba kuna njia mbili za kuondoka katika ulimwengu huu.
Ningeweza kuuacha ulimwengu huu, bila kitu chochote cha kuonesha kwamba niliishi hapa. Kama nalenga mambo ya ulimwengu huu, na sina macho kwa ajili ya mambo ya muhimu kwa ajili ya uzima wa milele, hivyo sina hazina iliyotunzwa, sina uzima ndani ya Kristo, hakuna cha kwenda nacho katika uzima wa milele.
Ama naweza kuwa mwanafunzi wa Yesu mwaminifu, nikifunza kumhusu yeye, na kujenga ghala la hazina zenye thamani ya milele. Naweza ishi katika njia ambayo nikienda nyumbani kwa Mungu, nitamsikia akinambia “Vyema, mtumwa mwema na mwaminifu” (Mathayo 25:14-30) Aina hii ya maisha pia huyafanya maisha duniani kuwa mazuri na yenye thamani, na maisha yangu yanaweza kuwa baraka na msaada kwa watu wengine.
Maisha yangu duniani.
Hivyo, najua kwamba maisha ninayoishi ninapokuwa hapa duniani, yatapima namna nitakapokutana na kifo muda wangu wa kufa utakapowadia. Kama ninaishi kwa uaminifu, kuyashinda maisha na ninaheshimu neno la Mungu, hivyo naweza kukutana na kifo kwa furaha na amani. Kifo si kitu cha kuogopa kama mimi ni mwanafunzi wa Yesu. Ninaweza kukutana na kifo kwa furaha nikitarajia kupata ujira wangu. Naweza kubadilika kabisa kutoka kuwa mwenye hofu juu ya kifo kuwa mtu ambaye hufikiria juu ya kifo kama ambavyo Mungu hufanya – ambavyo ni kuwa pamoja nae.
Katika kitabu cha Mathayo 25:34 Yesu anatwambia, “Njooni mliobarikiwa na baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa kwa ulimwengu” Na 1Yohana 2:25, “Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidi, yaani uzima wa milele.”
Njia nzuri ya kuwa tayari kukutana na Mungu tunapokufa, ni kumjua ingali tu hai. “mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi”. Yakobo 4:8. “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Wafilipi 4:6-7. Hivyo naweza kuitazamia siku tutakayokutana na baba yetu pamoja na mwanae, Yesu tuliyejifunza kumjua na kumpenda tulipokuwa bado tukiwa hapa duniani.
Neno la Mungu ni la kweli.
Nimeona kwamba neno la Mungu limethibitishwa kuwa kweli kwa njia nynigi katika maisha yangu. Ninaamini kwamba ahadi zake kuhusu uzima baada ya kifo zitakua kweli na tukufu. “Ahadi ya Bwana imehakikishwa, yeye ni ngao yao. Wote wanaomkimbilia.” Zaburi 18:30. Nimekuwa na fursa nyingi za kumjaribu Mungu, na amethibitisha mwenyewe ukweli kila wakati. Neno lake limekuwa msingi wa uhakika maishani mwangu.
Imeandikwa katika Biblia kwamba siku zetu zilihesabiwa kabla ya ulimwengu kuanza. Mungu amepanga mambo ya kufanya kwa ajili yetu. Anajua ni muda kiasi gani tunao hapa duniani, na ni muda unaomtosha kukamilisha kazi aliyoianzisha ndani yetu. (Wafilipi 1:6) tunapaswa kuishi kwa thamani ya wito huu mkuu na mtakatifu. Nikiamini kilichoandikwa katika Biblia, nina tumaini ndani yake na kujisafisha mwenyewe kama yeye alivyo msafi. (1Yohana 3:3)
Wazo kuu ni: kama ninaamini kilichoandikwa katika Biblia na ni mwaminifu katika kutii neno la Mungu kama lilivyoandikwa, sitaogopa kifo bali nitatazamia kumsikia Yesu akisema, “Vyema, mtumwa mwema na mwaminifu,….. ingia katika furaha ya bwana wako.” Mathayo 25:21-23.