Mipaka iliyowekwa na Mungu: Kusudi lake na maisha yetu

Mipaka iliyowekwa na Mungu: Kusudi lake na maisha yetu

Mungu mwenyewe ndiye anayedhibiti mipaka ya maisha yetu kwa lengo la kutusogeza karibu naye.

16/2/20254 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Mipaka iliyowekwa na Mungu: Kusudi lake na maisha yetu

Mungu anataka kutuleta karibu naye

Sisi sote tuna mipaka katika maisha yetu. Mipaka ni hali zetu, mahali tunapoishi, afya zetu, fedha zetu, na kadhalika. Mipaka au hali hizi zinaweza kubadilika wakati wa maisha yetu. Wakati fulani tunaweza kuzibadilisha sisi wenyewe na wakati mwingine hali ambazo ziko nje ya uwezo wetu zinaweza kuzibadilisha. Tunaweza kupoteza sehemu kubwa ya maisha yetu kutamani mipaka yetu iwe tofauti - wakati kwa kweli ni muhimu zaidi jinsi tunavyoishi ndani yake.

Paulo alisema katika Matendo 17:26-27: “Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.” Kwa hiyo mwishowe, ni Mungu ndiye anayedhibiti mipaka katika maisha yetu na lengo lake katika kufanya hivyo ni kutuleta karibu naye.

Ayubu alijifunza nini mipaka yake ilipobadilika

Mipaka (hali) ya Ayubu ilibadilika sana wakati wa maisha yake. Kwa ruhusa ya Mungu, Shetani aliharibu mali zote za Ayubu na kuwaua watoto wake 10 kwa siku moja. (tazama Ayubu 1.) Kwa kushangaza, hili lilikuwa jibu la Ayubu: “Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia;  akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe.  Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.” Ayubu 1:20-22.

Kisha mipaka ya Ayubu ikawa midogo zaidi Mungu alipompa Shetani ruhusa ya kuugusa mwili wake: “Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Ayubu 2:7.

Mke na marafiki wa Ayubu walikuwa na hakika kwamba Ayubu alikuwa amemchukiza Bwana, lakini Ayubu alielewa kujiweka karibu zaidi na Mungu katika wakati huu, ili baadaye angeweza kusema: “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu.” Ayubu 42:5-6. Alitumia mabadiliko hayo katika mipaka yake ili kupata uhusiano wenye nguvu zaidi pamoja na Mungu.

Uhusiano wa kudumu na Mungu

Chaguo hili la kujiweka karibu zaidi na Mungu katika majaribu ya maisha, na katika mipaka iliyobadilishwa ambayo majaribu haya yanaweza kuleta, ni jambo ambalo mashujaa wa imani kama Nuhu, Ibrahimu, Musa n.k wamefanya katika vizazi vyote. (Tazama Waebrania 11.) Walikubali kwa furaha mabadiliko haya ya mara kwa mara yasiyopendeza na walipata uzoefu wa “…kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Waebrania 11:6.

Pia Paulo aliandika jinsi alivyojifunza kukabili hali kama hizo maishani mwake: “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Wafilipi 4:12-13.

Tunapotazama mipaka na hali zetu kwa njia hii, tutaona yale ambayo Yesu alisema: “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” Yohana 17:3. Maisha yanakuwa ya kuvutia tunapoishi maisha yetu pamoja na Mungu, ambaye anatumia kila kitu tunachopitia ili kutuleta katika uhusiano wa kina zaidi Naye na Mwanawe, ambao hutupelekea kuwa zaidi kama Yesu. (Warumi 8:28-29.)

Hatutapoteza tena muda kutumainia mabadiliko katika mambo ya kidunia ambayo hayawezi kamwe kuleta utakaso wa kweli, lakini afadhali tutapata maisha ya kimbingu ambayo pia yanamaanisha ushirika wa kweli na wengine ambao wana lengo hili sawa.

Chapisho hili linapatikana katika

: Makala haya yanatokana na makala ya Steve Lenk yaliyochapishwa awali kwenye https://activechristianity.org/ na yamebadilishwa kwa ruhusa ya matumizi kwenye tovuti hii.