Kumdharau mtu wa hali ya chini ni kumtukana Mungu

Kumdharau mtu wa hali ya chini ni kumtukana Mungu

Tunavyofikiria na kuwatendea wahitaji, wanyonge na wale ambao ulimwengu huwadharau, inaonesha tunachofikiria juu ya Mungu, Muumba.

8/6/20203 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Kumdharau mtu wa hali ya chini ni kumtukana Mungu

4 dak

“Amwoneaye maskini humsuta  muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.” Mithali 14:31

Mungu hamdharau mtu

 Katika asili yetu ya kibinadamu (ambayo pia huitwa mwili) kuna hamu ya kuonekana na kuheshimiwa. Mara nyingi, hamu hii ni kubwa sana, kiasi kwamba watu hawajali ikiwa watalazimika kumtendea mtu mwingine isivyo haki, maadamu wanapata heshima.

 

Kwa kawaida wadhaifu na wenye uhitaji ndiyo hutendewa mabaya na visivyo haki, na mara nyingi, hawana watu wengi wanaowatetea na kusimama kwa ajili yao, kwa sababu watu wengi humtazama mtu aliye mkubwa au muhimu. Masikini hajajiumba mwenyewe. Kwa hivyo, kumtendea mabaya na isivyo haki ni kumtukana au kumkosoa Mungu, Muumba wake. Lakini “Mkombozi wao ni hodari; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.” Yeremia 50:34

 

Mungu huadhibu dhuluma zote. Kwa hivyo ni muhimu kuwa waangalifu zaidi jinsi tunavyowatendea wengine. Rehema huzidi hukumu. (Yakobo 2:13.) Paulo anaandika, “Tupeni nafasi mioyoni mwenu. Hatukumdhulumu mtu yeyote, wala kumharibu mtu, wala kumkaramkia mtu. 2Wakorintho 7:2.  Aliogopa kuumiza mtu yeyote ambaye Yesu alimfia.

 

“Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo  kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri  vina uzuru zaidi...” 1 wakorintho 12:23. Mtu akiteseka au kuumia kwa sababu unamtania au unamdhihaki mbele ya wengine, unamtukana Mungu aliyemuumba. Kwa maana Mungu anasema katika Neno lake kwamba unapaswa kumlinda. “Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu yeyote; Ana uweza katika nguvu za fahamu.” Ayubu 36:5. Ni nani anayeweza kujilinganisha na Mungu? Ni nani anayeweza kuelewa vitu kama vile Mungu anavyovielewa? Nani anajua udhaifu wetu wote kama anavyojua yeye? Na bado hana dharau kwa mtu yeyote.

Wafanyakazi wa Mungu katika kubariki na kusaidia watu

 Ikiwa tuna mtazamo kama wa Yesu, na tunanyenyekea na kuwaza mema juu ya wengine kuliko sisi, tutaweza kusaidia na kubariki watu. Mungu huwajali sana wanyonge na wenye hali ya chini “BWANA Mungu asema hivi, Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haipaswi wachungaji kuwalisha kondoo?... mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema bwana Mungu.” Ezekieli 34:2,15 

 Mungu aliwakasirikia wachungaji wa Israeli kwa sababu hawakuwa wamewalinda na kuwatunza wanyonge, hawakuwaponya wagonjwa, hawakwenda kutafuta wale waliopotea na kuwarudisha. Tupendane, ambayo ndiyo dhamana kamili inayotuweka pamoja (Wakolosai 3:14) na kuwa wafanya kazi wa Mungu ili wanyonge na wadhaifu waweze kukua na kujawa na furaha katika kanisa la Mungu. Ikiwa tutafanya hivyo, tunamheshimu pia Mungu, ambaye ndiye Muumba wa kila mtu na kila kitu.

Chapisho hili linapatikana katika

Sifa: Nakala hii inategemea nakala ya Kaare J. Smith ambayo ilionekana mara ya kwanza chini ya kichwa "Dharau kwa watu wa hali ya chini" katika jarida la mara kwa mara la BCC "Skjulte Skatter" ("Hazina Iliyofichwa") mnamo Desemba 1970. Imetafsiriwa kutoka kwa Kinorwe na imebadilishwa kwa matumizi kwenye wavuti hii. © Hakimiliki Stiftelsen Skjulte Skatters Forlag