Hivi karibuni, nimegundua namna nilivyoweza kujiona mwenyewe kuwa bora kiasi kuliko watu wengine ambao wasingeweza kuwa werevu kama nilivyo, kufanya mambo tofauti ama kutoona vitu kwa namna navyoviona. Baadhi ya watu wanaweza kujilinganisha na watu wengine na kukuza hali ya uduni – ambapo hujihisi wenye thamani kidogo kuliko wale wanaowazunguka. Lakini nimegundua ndani yangu kwamba ninapojilinganisha na wengine, mara nyingi huwa naishia kujiona nikiwa na hali ya ubora - nikifikiria kwamba niko bora kuliko wale wanaonizunguka.
Kushindana na wengine “walio na kila kitu”
Nimeona hili hata katika mambo madogo madogo katika Maisha. Kwa mfano, siendani na mtindo. Hata kama napenda kuwa na nguo mpya, siyo muhimu sana kwangu hivyo huwa naishia kujikuta nikivaa nguo ambazo zinaweza kuwa za mtindo wa miaka michache iliyopita. Lakini kuna wengine ambao huishia kuvaa vitu, wana majumba makubwa na magari mazuri.
Kutazama watu ambao wana vitu zaidi yangu kunaweza kunifanya nijihisi duni ama kujihurumia. Kujaribu kuendelea na hali hii inaweza kunisababishia msongo wa mawazo na wasiwasi na kuwa na uhitaji, Pamoja na kutokuwa na furaha kwa kutokuweza kushindana na hawa akina mama wenye “kila kitu”
Lakini pia nimehisi upande wake mwingine, ambao ni kujihisi bora, kujihisi bora kidogo kuwaliko. Baadhi ya mawazo yaliyokuja ni, “vipi ulimwenguni anapata muda wa kufanya kile,” au “Mimi siyo bure, kwa sababu sijali kama navaa nguo ile ile mara kwa mara niendapo kanisani,”au “Wanataka kuthibitisha nini kwa kuchapisha kile kwenye Instagram?” orodha huendelea na kuendelea.
Matokeo ya wivu
Kuwakosoa wengine, hata kama ipo tu katika fikra zangu, ni sawa na kufikiria kwamba mimi ni bora kuliko wengine. Hata kama nitagundua baadaye, fikra hizi mara huwa ni kwa sasbabu nina wivu. Na ni muhimu kuliona hili na kulikubali mwenyewe. Nina uzoefu kwamba fikra hizi za wivu ni zaidi kama ugonjwa wa kuambukiza, zinaleta machafuko katika Maisha na pia husambaa kwenye Maisha ya wale nilio karibu nao.
Imeandikwa katika kitabu cha Yakobo 3:16 “Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.” Wivu husabisha nilinganishe nilichonacho na mtu mwingine na kwa siri natamani ningekuwa na kile walichonacho, au hata kutamani ningekua na kitu kizuri kuliko wao hivyo wangekuwa na wivu dhidi yangu.
Ilivyo kama wazimu, kuhisi kwamba sina kile ambacho mtu mwingine anacho hata kunisababisha nimdharau mtu huyo. Naweza fikiri, “Kwa nini wanatumia pesa kwa ajili ya kile”, Kiukweli ningekua na pesa ningeweza kununua kitu kilekile. Kama ilivyoandikwa kwenye neno la Mungu, wivu husababisha mkanganyiko (Kukosa utulivu), na imefungamana na kila aina ya uovu.
Kuuweka moyo wangu safi
“Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima” Mithali 4:23. Mambo ninayoyaruhusu kuingia moyoni mwangu na akilini mwangu yanaweza kuleta amani na joto, ama machafuko mengi, mawazo yasiyo na furaha na wasiwasi. Kwa kufanya neno la Mungu, na kujua kuchagua kutokubaliana na mawazo hasi, ninaweza kuuweka moyo wangu safi. Hivyo sishawishiwi na kutawaliwa na maoni na fikra, na hisia ambazo hunijia, na naweza kuwaona wengine katika uzuri na nuru yenye baraka.
“Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake” Wafilipi 2:3.
Endapo nitafanya kama kifungu hiki kinavyosema, nitajiokoa kutoka kwenye maoni makuu juu yangu mwenyewe na kuwadharau wengine. Badala ya kutazama nje kila mara, wanachofanya wengine, na kuhukumu kwa kuangalia mambo hayo, ninaweza kuwa na moyo wenye joto na uliofunguka. Naweza kujifunza kuwabariki wengine na kuwafanyia mema iwezekanavyo.