Tukitembea katika nuru, tuna ushirika katika mwili wa Kristo

Tukitembea katika nuru, tuna ushirika katika mwili wa Kristo

Ni upendo katika Roho unaouunganisha mwili wa Kristo duniani.

17/11/2026—3 dk

Written by Johan Oscar Smith

Tukitembea katika nuru, tuna ushirika katika mwili wa Kristo

“Lakini tukienenda katika nuru, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu ya Yesu Mwana wake hutusafisha dhambi yote.” 1 Yohana 1:7.

Ushirika katika mwili wa Kristo

Tukitembea katika nuru, tuna ushirika sisi kwa sisi. Ndipo maisha yetu huwa mazuri sana, Shetani anasetwa chini ya miguu yetu, na sisi hupendana kweli kweli.

Lakini ni lazima tuwe macho sana ili kuiendeleza nuru hii, upendo na ushirika katika Roho. Hata wivu kidogo, shaka kidogo kuhusu ndugu, kutokuwa na fadhili kidogo au kusemezana kunaweza kumpa Shetani nafasi ya kuingia. Hivyo kila mmoja wetu ni lazima afanye kazi kwa bidii kumseta Shetani chini ya miguu yetu. Tukifanya hivi, Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu ya kanisa, ambalo ni mwili wa Kristo (Warumi 16:20).

Kila mmoja wetu anapojitahidi kwa bidii kuzishika amri za Kristo bila mawaa (1 Timotheo 6:14), hiyo inakuwa ngome imara katika vita vya kanisa dhidi ya nguvu za uovu.

Tunapozitii amri za Yesu na kuiacha asili yetu ya dhambi ikiwa imesulubiwa, hili, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kupitia uaminifu na upendo kwa Baba na Mwana, litatuweka pamoja katika umoja usiotikisika ndani ya mwili wa Kristo. Hili ndilo kanisa, ambamo viungo husaidiana kupitia kila kifungo ambacho Mungu hutoa. Kwa njia hii mwili wote hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, kila sehemu ikifanya kazi ambayo imepewa kuifanya (Waefeso 4:16).

Kiungo kimoja peke yake si mwili mzima, bali viungo vyote pamoja huunda mwili. Mungu aliupanga mwili pamoja kama alivyotaka ili tuweze kujifunza kuvumiliana sisi kwa sisi na kupokea msaada kutoka miongoni mwetu sisi ambao Kristo, kwa neema na zawadi zake, amempa kila mtu kwa ajili ya kukua kiroho.

Sheria za mwili wa Kristo

Lakini Shetani anapoingia, analeta mgawanyiko. Msaada wa kiroho kutoka kwa kila kiungo hutenganishwa na mwili hauwezi kufanya kazi. Hili linaweza kuepukwa ikiwa kila kiungo cha mwili kingependelea kuteseka badala ya kuingia katika dhambi. Kwa dakika tano tu unaweza kusema uovu mwingi kiasi kwamba hata miaka mitano haiwezi kuponya ushirika uliovunjika na kurudisha imani.

Mikutano ya Kikristo isiyoujua ushirika huu mtukufu katika Roho pia haijui sheria takatifu zinazofanya kazi ndani ya mwili, kwa sababu bado mwili haujaundwa. Hukutana katika ibada za kanisa na kisha huondoka tena kama watu wanaojuana tu kwa njia ya kawaida, ya kibinadamu kulingana na mwili. Mahusiano kama hayo ni ya juu juu sana.

Paulo alisema, “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena.” 2 Wakorintho 5:16. Kumjua Bwana ni kuwa roho moja pamoja naye. Ni upendo katika Roho unaokuwa nguvu ya kuunganisha ndani ya mwili wa Kristo duniani.

Basi na tujifunze kutembea kwa uangalifu katika kanisa la Mungu aliye hai, ambalo ni mwili wa Kristo (Waefeso 5:15).

Chapisho hili linapatikana katika

Makala hii ya Johan O Smith imetafsiriwa kutoka Kinorwe, na ilichapishwa kwa mara ya kwanza chini ya kichwa "If we walk in the light" katika jarida la BCC "Skjulte Skatter" ("Hazina Zilizofichwa") Aprili 1940. Imebadilishwa kwa ruhusa kwa ajili ya matumizi kwenye tovuti hii.

© Hakimiliki Stiftelsen Skjulte Skatters Forlag