Mwanzoni mwa ndoa yetu, tuliishi na wenzi wa ndoa wanaomcha Mungu kwa miezi michache. Wanandoa hawa walikuwa na watoto kadhaa na sio pesa nyingi. Nyumba na samani zilikuwa za zamani, watoto walikuwa wakicheza kila mahali na kufanya fujo, walifuga Wanyama kadhaa na kila wakati walionekana kuwa wageni.
Siku moja nilikuwa nikinywa chai na Mama, aliniambia, "Tunaishi kama wafalme…"
Siku hiyo alinionesha siri kubwa: Kushukuru ni njia ya kufikiria, sio matokeo ya hali. Na hapa kuna jambo: tunapojifunza kuwa na shukrani kunaweza kubadilisha maisha yetu ndani ya sekunde.
Kweli, kivipi?
Shukrani inapaswa kuwa msingi wa maisha yetu ya kila siku, na kuna sababu zake nzuri.
Sababu moja ni kwamba inaathiri watu wanaotuzunguka. Tulikuwa na mgeni hivi karibuni na tulipanga kuifanya siku yake iwe njema. Lakini mambo hayakuwa kama tulivyotarajia. Kabla sijajisikia vibaya kwamba siku haikwenda vile vile tulivyopanga, namna mgeni wetu alivyoitikia ilichukua nafasi. Kila kitu kilikuwa "sawa" kwake - alikuwa na furaha kwa kila jambo; alicheka mambo yalipokwenda vibaya na alikuwa akiongea na sisi kwa furaha kwenye msongamano wa magari. Shukrani yake ilinifurahisha na ilikuwa mfano kwangu jinsi tunavyoathiriana, na jinsi shukrani inaweza kubadilisha hali kuwa nzuri.
Na kushukuru kunatubadilisha sisi pia. Kuna wakati nilitumia Neno la Mungu kuhukumu kile mume wangu alikuwa akifanya na kusema, badala ya kutumia Neno la Mungu kujihukumu mwenyewe. Hii wakati mwingine ilisababisha kushtakiana, na nakumbuka siku moja alikuwa amesema neno lililoniumiza na nilikuwa nimeudhika. Nilitembea hadi dirishani na kumtazama akienda kazini na ghafla nilifikiri: Yeye ni mtu mzuri, kweli. Na niliamua kuweka mashaka yangu pembeni na kumuombea - kwamba afike kazini salama, kwamba siku yake iende vizuri, aweze kusikia sauti ya Roho katika yote aliyoyafanya, na kwamba ningeweza kuchukua sehemu yangu kutengeneza nyumba yenye amani.
Nilipokuwa nikimwombea, nilizidi kuwa mwenye shukrani kwa ajili yake, na hasira yangu ilionekana kuwa ndogo na ya kijinga. Mabadiliko kutoka kwenye kukerwa na kushukuru yalichukua sekunde tano lakini yalibadilisha kabisa siku yangu na jinsi nilivyoyatazama maisha. Nilianza kuacha kumhukumu.
Lakini ni nini hasa hutokea katika sekunde hizo tano muhimu sana?
Kuna wakati ambapo Mungu hufungua macho yangu na kujiona jinsi mimi mwenyewe nilivyo, na pia ninapata hamu ya kuibadilisha. Kile ninachofanya katika sekunde hizo kitaamua ikiwa nitatumia nafasi hiyo kubadilishwa kwa nguvu ya Roho, au ikiwa nitatoka dirishani bado ninaamini mume wangu amekosea…
“Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukirudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye roho. " 2 Wakorintho 3:18 .