Siri rahisi ya kuendelea kuwa mnyenyekevu

Siri rahisi ya kuendelea kuwa mnyenyekevu

Aya hii ni kama mapatano kati yangu na Mungu: “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

2/2/20215 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Siri rahisi ya kuendelea kuwa mnyenyekevu

8 dak

"Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema." 1 Petro 5:5-6. Je, hii ina maana gani hasa katika maisha yangu ya kila siku?

Binafsi, nimegundua kwamba siku zote ninajifikiria sana. Hapa kuna baadhi ya mifano ya kile ninachoweza kujikuta nikifikiria: "Niko sawa - njia yangu bila shaka ndiyo njia sahihi." "Mtu huyo anahitaji kusikiliza maoni yangu hivi sasa." “Kwa nini huwa wanasema hivi au vile? Inaonyesha kwamba wanafikiria vibaya tu."

Ninaweza kuwa nikijishughulisha sana na haya yanayoitwa mambo ya "kawaida", mawazo ya asili, kwamba ni vigumu kwangu kuona kwamba yote yanaonyesha wazi jinsi ninavyojivuna!

Nina makosa

Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema…” Warumi 7:18. Biblia inatuambia kwamba kila mwanadamu amezaliwa na asili ya dhambi, na Paulo anasema katika barua zake kwamba hakuna kitu chema kinachoweza kutoka kwenye asili hiyo ya dhambi.

Tutaona mambo katika asili yetu ya kibinadamu ambayo yapo kinyume na mapenzi ya Mungu. Kwa mfano, tamaa ya kuwa tajiri, kuwa na mamlaka au mafanikio katika ulimwengu huu ni kinyume cha mapenzi ya Mungu moja kwa moja, kwa sababu mapenzi ya Mungu kwetu ni kuwa wanyenyekevu wa moyo. (Mathayo 11:28-30.) Au tunaweza kuona mambo yapo kinyume na mapenzi Yake kabisa, kama vile hasira, kuudhika na kuwakosoa wengine.

Paulo anaandika katika Warumi 7 kwamba anachukia mambo haya anapoyaona. (Warumi 7:17.)

Nia yake yote ilikuwa kufanya mapenzi ya Mungu tu, na katika sura hii tunapata kuona jambo fulani la mapambano haya kati ya nia yake ya kutenda mema, na uovu ambao aliuona ndani yake mwenyewe.

Hata ikiwa ni kawaida kwa wanadamu kuwa na mawazo na mielekeo yenye dhambi, hiyo haimaanishi kwamba ni lazima ibaki hivyo! Yesu alituwezesha sisi kuwa huru kutokana na mawazo haya, na Paulo anaandika zaidi, “Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili , mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa roho, mtaishi.” Warumi 8:12-13.

Roho wa Mungu anatuonyesha kwa upole maeneo katika maisha yetu ambayo Mungu hataki yawe. Mungu anaponionyesha mambo haya na ninapata kuyaona kwa uwazi zaidi, ninaweza kufanya jambo dhidi yake. Ninaweza kumwomba Mungu anisaidie kuyakataa mawazo haya yanayotokana na mapenzi na matamanio yangu, na badala yake kuchagua kutenda yale yaliyoandikwa katika Neno la Mungu na kile ninachojua ni mapenzi Yake. Hii ndiyo maana ya kujinyenyekeza. Ninapoendelea kufanya hivi, ninakuwa huru zaidi na zaidi kutoka kwenye mapenzi na tamaa zangu, ambazo ninazichukia kwa sababu ni kinyume na kile ambacho Mungu anataka.

Kwangu, hii yote ina maana kwamba ni lazima nijisalimishe mwenyewe kwa Mungu na kumngojea. Siwezi kuendelea kubaki na kiburi na mawazo makubwa juu yangu mwenyewe ikiwa ninaelewa kwamba " ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema ". Bila shaka, hii haimaanishi kwamba ninapaswa kukata tamaa au kufadhaika kuhusu hili pia, kwa sababu hayo pia si mapenzi ya Mungu kwangu.

Hapana, Mungu anataka kunibadilisha ili niwe huru kabisa kutokana na uovu ulio katika asili yangu ya kibinadamu. Ili kufanya hivi, Ananionyesha maeneo ambayo yanahitaji kubadilika na atanipa neema na msaada wote ninaohitaji kuwa huru. Kuwa mnyenyekevu kunamaanisha kwamba ninaamini jinsi Mungu anavyofanya kazi nami kunionyesha maeneo haya tofauti na kwamba ninamwamini atanipa neema na msaada wote ninaohitaji kufanya mambo kwa njia tofauti.

Wengine wana makosa pia

Kadiri muda unavyosonga, naona kwamba kuna mengi katika asili yangu ya kibinadamu ambayo hayampendezi Mungu vyema, na ninaanza kuona jinsi ambavyo Mungu amekuwa na subira na rehema kwangu! Hili linanifundisha kwamba mimi pia ni lazima nionyeshe rehema na huruma hii kwa wengine. Paulo anaandika, “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” Warumi 8:1.

Ninaweza kufikiri kwamba kile ambacho watu wengine wanafanya au kusema si sahihi na kwamba ninajua namna wanavyopaswa kutenda au kusema kwa njia tofauti, lakini Roho wa Mungu hafanyi kazi hivyo. Badala yake, Ananifundisha kuwa mvumilivu na kuvumilia makosa ya wengine kwa unyenyekevu na huruma. Hii ndiyo sababu tumepewa amri rahisi kutoka kwa Mahubiri ya Mlimani, “Msihukumu,msije mkahukumiwa ninyi.” Mathayo 7:1-2. Maneno haya yamejaa hekima sana. Hebu fikiria jinsi ulimwengu ungekuwa na amani zaidi ikiwa kila mtu angeamini maneno haya na kuyatenda!

Wakati huo huo, Roho atanionyesha makosa yangu mwenyewe - kutokuwa na subira kwangu, ambapo ninahukumu wengine au kiburi changu - na Yeye atanionyesha jinsi ya kushinda. Katika hali zangu, ninahitaji kuzingatia mahali ambapo mimi mwenyewe ninahitaji kubadilika. Kisha, nikiona mambo kwa wengine niweze kuzungumza nao kuhusu mambo hayo kwa upendo wa kweli, inaweza kuwa baraka kusema jambo fulani. Hata hivyo, ni suala tofauti ikiwa ninazungumza nao kuhusu makosa yao kwa kuudhika, hasira au mawazo yangu ya kiburi.

Kiburi mara nyingi ni kitu kilichofichwa sana. Ninakiona katika namna ninavyojifikiria, jinsi ninavyofikiri juu ya wengine na jinsi ninavyomruhusu Mungu afanye kazi maishani mwangu. Lakini kuna aya ambayo ni kama mapatano kati yangu na Mungu: "Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema." Nisipokuwa mwangalifu na kuendelea na mawazo haya yote ya kiburi, Mungu atanipinga. Ni jambo la hatari sana kwa Mungu kuniondolea neema yake maishani mwangu, kwa sababu tu sikutaka kujinyenyekeza!

Lakini ikiwa nitajisalimisha kwa Mungu katika kila kitu - ikiwa nitamruhusu kuwa kichwa changu na kiongozi wangu, na kukubali kwamba amenipa kila kitu na atanipa msaada wote ninaohitaji - basi nitapata neema juu ya maisha yangu! Kwa kweli hilo ni jambo la kutazamia!

Chapisho hili linapatikana katika

Makala haya yanatokana na makala ya Page Owens yaliyochapishwa awali kwenye https://activechristianity.org/ na yamebadilishwa kwa ruhusa ya matumizi kwenye tovuti hii.