“Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” Yohana 17:20-23.
Mungu na Yesu ni kitu kimoja kwa namna gani?
Tuna wito mkuu na mtakatifu wa kuwa kitu kimoja kama Baba na Mwana walivyo kitu kimoja. Ikiwa tunataka kuwa kitu kimoja kama wao, lazima tumfuate Mwana katika njia nyembamba inayoelekea kwenye uzima.
“Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” Yohana 6:38.
“Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza kutii kwa mateso yale aliyopitia. Naye alipokwisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii.” Waebrania 5:8-9.
Hapa tunaweza kuona jinsi Baba na Mwana walivyokuwa kitu kimoja. Yesu alizaliwa katika jamii ya wanadamu na akawa Mwana wa Adamu (1 Timotheo 2:5). Kama Mwana wa Adamu, kama mwanadamu, alijifunza kutii. Haikuwa rahisi kwake, lakini alijifunza kupitia mateso, na katika Isaya 53 tunasoma kuhusu baadhi ya mateso ambayo kupitia hayo alijifunza kutii.
“Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.” Isaya 53:10.
Yesu aliomba, “Sio mapenzi yangu, bali yako yatimizwe!” Luka 22:42. Haya “mapenzi yangu” yalikuwa mapenzi ya jamii ya wanadamu, mapenzi ya Yesu kama Mwana wa Adamu. Mapenzi haya yalipaswa kusagwa ili mapenzi ya Bwana yaweze kutimizwa kupitia Yeye, na hapa Yesu ilimbidi awe dhabihu. Alienda katika njia hii kwa hiari yake mwenyewe. Aliichagua! Hii ilikuwa njia mpya na iliyo hai ambayo aliitufungulia ili tumfuate (Waebrania 10:20). Hii ilikuwa njia ambamo mapenzi ya mwanadamu yalisagwa na ambamo utimilifu wote wa asili ya Mungu ulikuja kuishi katika umbo la kibinadamu (Wakolosai 1:19; Wakolosai 2:9).
Tumepokea ahadi kuu na za thamani kupitia kumjua Yeye, ili tuweze pia kushiriki katika asili ya Mungu (2 Petro 1:3-4).
Tunakuwa kitu kimoja kwa namna gani kama Baba na Mwana walivyo kitu kimoja?
Leo tuna nafasi zilezile ambazo Yesu alikuwa nazo ikiwa nasi tuko tayari kuwa dhabihu. Yesu akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii (Waebrania 5:9). Katika njia hii tunakuwa kitu kimoja kama Baba na Mwana walivyo kitu kimoja.
Hili ni jambo la muhimu sana kiasi kwamba Paulo anasema ilikuwa kwa sababu hii kwamba alipokea neema na utume ili kuwaongoza watu kutoka mataifa yote katika utii utokanao na imani (Warumi 1:5). Lakini haiwezekani kujifunza utii bila kuwa tayari kusagwa, bila kuwa tayari kuteseka.
Kuna watu wengi wanaojaribu kuwafanya makundi mbalimbali ya dini kuwa kitu kimoja, lakini haina maana. Viongozi wanajiona kuwa wakuu, wana maoni yao makali, na wanachama wanaowafuata hufanya hivyo hivyo. Ndiyo maana kuna mapigano daima na uchungu ndani ya makundi mbalimbali ya dini na kati yao. Hawataki kusagwa. Wengi wao huzungumza kuhusu upendo na husoma 1 Wakorintho 13, lakini huwezi kupata upendo huu bila kuwa tayari kusagwa, bila kuacha kiburi chako mwenyewe na maoni yako makali.
Vivyo hivyo tunaweza kusoma yale ambayo upendo haufanyi: hauhusudu, haujivuni, hautafuti yaliyo yake mwenyewe, hauwi mchungu, haufikiri mabaya, n.k. Watu wasiotaka kusagwa huwa wachungu, hutafuta yaliyo yao wenyewe, na hujivuna. Watu kama hao hawawezi kamwe kuwa kitu kimoja. Daima huonekana kuwa na sababu ya kukasirika badala ya kuchukua msalaba wao, kujikana wenyewe, na kuhukumu ubinafsi wao na ugumu wao wenyewe.
Pia tunasoma yale ambayo upendo hufanya: huvumilia; hufurahi katika kweli na hustahimili mambo yote; huamini yote, hutumaini yote, na huvumilia yote (1 Wakorintho 13:4-7; Wakolosai 3:12-14). Wakati wengine wanakuwa wagumu na wakaidi, watu wengi husema: “Mimi sitaweza kuvumilia hilo. Lazima kuwe na mpaka wa kile ambacho mtu anapaswa kustahimili.” Badala ya kuruhusu wasagwe, huwa wagumu na kujitetea wenyewe pamoja na haki na maoni yao wenyewe. Badala ya kusamehe kama Yesu alivyotusamehe sisi, huwa waovu, na huzungumza vibaya kuhusu ndugu yao wa kiume au wa kike.
Huenda humpendi mtu fulani, lakini ingawa bado una adabu na unatabasamu, unajitenga naye. Hutaki kuwa na ushirika katika Roho pamoja naye. Kiburi chako hakiwezi kumvumilia mtu mwingine alivyo. Hutaki kiburi chako kisagwe ili upate upendo unaovumilia yote na kutumaini yote. Bila shaka hutaki kubishana naye, kwa hiyo unajitenga kwa adabu. Lakini hili si kuwa kitu kimoja kama Baba na Mwana walivyo kitu kimoja.
Kutimizwa kwa sala ya Yesu kwa ajili ya umoja wa Kikristo
Heri wale ambao wameelewa jinsi Mwana alivyo kitu kimoja na Baba, na ambao wanataka kumfuata Mwana katika njia hii mpya na iliyo hai. Sala ya Yesu inatimizwa katika maisha yao, nao daima wanakuwa katika utukufu pamoja. Hutembea katika nuru kama Yeye alivyo katika nuru, na damu ya Yesu huwasafisha dhambi yote. Wanaushirika wao kwa wao. (1 Yohana 1:7.)
Shukrani kwa Mungu kwa wokovu huu wa utukufu, na kwamba tunaweza kushiriki ndani yake tunapokuwa tayari kuwa dhabihu, na kwamba watu wengi zaidi na zaidi wanaweza kushiriki ndani yake. Katika ushirika huu katika nuru, Shetani hawezi kuingia.