“Lakini tukienenda katika nuru, kama yeye alivyo katika nuru, tuna ushirika sisi kwa sisi, na damu ya Yesu Kristo, Mwanawe, yatusafisha dhambi yote.” 1 Yohana 1:7.
Nuru ni nini? Tunaweza kupata jibu katika Zaburi 119:105: “Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu.”
Nuru ni nini?
Neno la Mungu ni nuru. Na kutembea katika nuru ni kuishi maisha yangu kulingana na Neno la Mungu – basi Neno huwa maisha yangu. Inamaanisha pia kwamba sifanyi chochote ambacho ni kinyume na Neno la Mungu.
Tunasoma katika 1 Yohana 1:5-6, “Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatufanyi iliyo kweli.” 1 Yohana 1:5-6.
Dhambi ni giza. Ukweli ni mwanga. Inaangaza ndani yangu na kunionyesha ambapo bado kuna dhambi katika maisha yangu. Nuru inapoangazia giza langu, ninapaswa kuukubali ukweli - kwamba bado kuna dhambi maishani mwangu ambayo ninahitaji kuiondoa. Neno la Mungu linanionyesha jinsi maisha yangu yanavyopaswa kuwa, na ninapojaribiwa kutenda dhambi, ninaweza kuchagua kufanya kile ambacho Neno la Mungu linasema badala ya kile ambacho tamaa zangu zinataka. Kwa njia hii, Neno linaweza kuwa uzima ndani yangu.
Nuru inanionyesha ukweli
Hebu tueleze kwa kutumia mfano. Labda nasikia kwamba mtu fulani amekuwa akinisema vibaya, na ninahisi kuumia, hasira, na kuudhika. Lakini basi nuru (Neno la Mungu) inakuja na kunionyesha kwamba ni kiburi changu mwenyewe na ubinafsi wangu ambao umeumizwa na kwamba ndiyo sababu halisi inayonifanya nihisi hasira na kuudhika, iwe kile walichosema kunihusu ni kweli au la.
Ukweli ni kwamba hasira yangu inatoka kwenye dhambi katika asili yangu ya kibinadamu, kutoka kwenye kiburi changu. Lakini Neno la Mungu linasema, “Waombeeni wanaowaudhi.” Mathayo 5:44; na, “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu Yakobo 4:6.
Sasa nuru imenionyesha giza ambalo bado liko ndani yangu - kiburi changu, kujihesabia haki, kutaka kusifiwa na watu. Ikiwa ningekuwa huru kabisa kutoka kwa hili, basi hakuna chochote ambacho mtu yeyote alisema juu yangu kinaweza kuniathiri hata kidogo. Sasa ninaweza kuchagua kutii nuru na kuchagua kufanya yale ambayo Neno la Mungu linasema, au ninaweza kuchagua kuendelea gizani.
Nikichagua kufanya kile ambacho Neno la Mungu husema, basi ninaruhusu damu ya Yesu Kristo kunisafisha kutoka kwenye dhambi (1 Yohana 1:7). Hiyo inamaanisha kuwa ninakubali ukweli, na nasema "hapana" kwa mawazo ya hasira na kujihesabia haki ambayo yanakuja - ninayapinga.
Huu ni mfano mmoja rahisi, lakini ninapotaka sana kufanya yale ambayo Neno la Mungu linasema, hunionyesha mambo mengine mengi ambayo bado yanahitaji kusafishwa maishani mwangu, makubwa au madogo. Bila nuru (Neno la Mungu) niko gizani na siwezi kuona ni kiasi gani cha dhambi katika asili yangu ya kibinadamu au jinsi ninavyohitaji kubadilika. Nuru huhukumu dhambi inayokaa ndani yangu, na ninapokuwa tayari kuhukumiwa na nuru, hatua kwa hatua, basi ninabadilishwa kuwa zaidi na zaidi kama Yesu (Warumi 8:29).
Tembea katika nuru - tii nuru
Watu wengi wanapendelea giza, kwa sababu hiyo ina maana kwamba hawapaswi kuacha dhambi. “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.” Yohana 3:19-21. Ubaya ni nini? Ni dhambi katika maisha yangu mwenyewe.
Ninapotembea katika nuru, maisha huwa huru na mazuri. Ninapotembea nuruni, dhamiri yangu huwa njema kila wakati. Ninapotembea katika nuru, nina ushirika na wengine kwa sababu mara tu ninapoona kitu ambacho kinaweza kuja kati yetu, mimi huchagua kufanya kile ambacho Neno la Mungu husema na sio uovu ambao asili yangu ya dhambi inataka.
"Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili Pamoja na Mawazo yake mabaya na tamaa zake." Wagalatia 5:24.
Ninapoipenda nuru, ninatamani iangaze katika kila sehemu ya maisha yangu ili niweze kuona mambo ambayo hayako jinsi Mungu anavyotaka yawe. Ninakuwa mtoto wa nuru. Ambapo mwanga huangaza, ukuaji mpya huanza. Upendo, furaha, fadhili, subira, na matunda yote ya Roho hukua katika nuru.
“Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika bwana; enendeni kama Watoto wa nuru." Waefeso 5:8.
Hata kama ninampenda Mungu, haimaanishi kwamba nina kiasi sawa cha nuru kama waumini wengine. Mungu ananionyesha kadiri niwezavyo kustahimili kwa wakati mmoja. Kwa hivyo siwezi kulazimisha nuru niliyopokea kwa mtu mwingine yeyote, iwe ni wanafunzi wao wenyewe au la. Nuru niliyopokea kutoka kwa Mungu ndiyo iliyo sawa kwangu. Siwezi kuwahukumu wengine kulingana na nuru yangu mwenyewe. Mungu pekee ndiye anayejua mioyo ya watu na anaweza kuhukumu kwa haki.
Wale wanaotembea katika nuru ni wanafunzi wa Yesu Kristo. “Kwa mara nyingine tena Yesu alisema na watu. Wakati huu alisema, “mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Yohana 8:12.
Ikiwa sisi ni wanafunzi wa kweli tunaomfuata Yesu katika nuru, basi 1 Yohana 1:7 yatakuwa maisha yetu: “bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”