Wale wapelelezi kumi na wawili walirudi kutoka kuipeleleza nchi ya Kanaani ili kumwambia Musa na wana wa Israeli juu ya kila kitu walichokiona. Watu walifurahi sana. Mungu mwenyewe alikuwa amewaongoza kutoka Misri, na hatimaye walikuwa wamefika kwenye mipaka ya nchi ya ahadi.
Siku 40 zilizopita Musa alikuwa amewatuma wale wapelelezi, na kuwaambia wachunguze kadiri wawezavyo kabla Waisraeli hawajaingia katika nchi na kuichukua iwe mali yao. Maneno yake kwao yalikuwa, “Jipeni moyo. Na mlete baadhi ya matunda ya nchi.” (Soma Hesabu 13 na 14.)
Na sasa walikuwa wamerudi, wakiwa wamebeba rundo la zabibu kubwa sana kiasi kwamba watu wawili walilazimika kulibeba kati yao! “Tulienda kwenye nchi uliyotutuma. Hakika inatiririka maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.” Kwa furaha watu walikusanyika ili wajionee wenyewe. Kila mtu alitaka kuwa na sehemu ya matunda.
Nchi ya ahadi
Katika Agano Jipya pia tunayo "nchi ya ahadi" ya kuchukua. Kama Wakristo tumepokea ahadi kuu kuliko zote: kuacgana na dhambi na kushiriki katika asili ya kimungu (2 Petro 1:3-4). Matunda ya nchi hii ni matunda ya Roho: upendo, furaha, uvumilivu, utu wema na amani. Nani hataki kuwa na vitu hivi?
Lakini furaha ya Waisraeli haikuchukua muda mrefu. Wapelelezi pia walikuwa wamewaona watu walioishi katika nchi: watu wenye nguvu walioishi katika miji yenye kuta zenye nguvu. Taarifa yao ilikuwa mbaya: "Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa na watu tuiowaona ndani yake ni warefu mno. … tukajiona nafsi zetu kama mapanzi; nao ndiyo walivyotuona.” Hesabu 13:32 (NCV).
Matokeo yake, watu wa Israeli walipoteza tumaini na kulia usiku kucha. Je! ndoto zao zote zilifikia hivi? Je! walikuwa wameteseka sana kwa taabu nyingi hivyo, na kusimamishwa moja kwa moja kwenye lango la nchi ya ahadi?
Je! unaamini, kama Yoshua na Kalebu?
Mara nyingi inaweza kuonekana hivyo katika maisha yetu ya Kikristo pia. Tunaacha maisha yetu ya zamani ili kumfuata Yesu, tukiwa na matumaini makubwa ya maisha bora. Lakini basi "adui" yetu, dhambi katika asili yetu, inaonekana kama jitu kubwa, na inaonekana haiwezekani kuishinda. Tunaanza kuhisi kwamba kuwa Mkristo kunagharimu sana; kwamba ni juhudi nyingi sana. Kwa nini Mungu hatusaidii?
Mungu hawezi kuwasaidia wale ambao hawataki kuamini. Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa upande mwingine, Yeye huwapa thawabu nyingi wale wanaomtafuta kwa dhati. (Waebrania 11:6 )
Yoshua na Kalebu, wawili kati ya wale wapelelezi, wakazungumza. “Ikiwa Bwana anafurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yeti … Lakini msimwasi BWANA. Wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuja juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi ; msiwaogope.” Hesabu 14:8-9.
Ungefikiri kwamba watu walijipa moyo, wakikumbuka ahadi za Mungu na miujiza waliyomwona akifanya kule jangwani. Lakini hapana. Kwa sababu ya kutokuamini, mambo yalipokuwa magumu na kuwaendea kinyume, walitaka kuwapiga mawe Yoshua na Kalebu, watu hawa wa imani, badala ya kupigana vita na kupigania nchi ya ahadi.
Imani ni chaguo
Lakini Mungu aliingilia kati. Kwa kutomwamini, watu wa Israeli walikuwa wakisema kwamba Mungu hana uwezo wa kuwasaidia. Mungu aliwakasirikia na kuapa kwamba hakuna mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka ishirini ambaye angeingia katika nchi ya ahadi – wote wangefia jangwani.
Kulikuwa na tofauti mbili: “Lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wake wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.... Kalebu, mwana wa Yefune, ataingia humo. Ndivyo atakavyokuwa Yoshua, mwana wa Nuni. Ni wao tu ndio watakaoingia katika ardhi. Hesabu 14:24,30.
Roho hii tofauti ilikuwa roho ya imani. Imani maana yake ni kutotazama kile unachokiona bali kuamini kuwa Mungu ni Mwenyezi. Imani inamaanisha kuwa mtiifu hata wakati ambapo huoni kitakachotokea. Imani maana yake ni tendo, kufanya jambo fulani. Imani huleta majibu.
Mungu anataka tuchague kuamini na kuchagua kutii. Anataka tufanye jambo fulani. Mungu alikuwa pamoja na Yoshua na Waisraeli wakati ambao, miaka 40 baadaye, wangeweza kuingia katika nchi ya ahadi, lakini walipaswa kuonyesha kwamba walitaka. Ilibidi wawe tayari kuipigania. Waisraeli walipoiteka Kanaani baada ya kuanguka kwa Yeriko, hakuna jiji moja lililotekwa bila kupigana.
Kuonja matunda
Katika roho ile ile ya imani ambayo Yoshua na Kalebu walikuwa nayo, tunapigana vita vyetu wenyewe dhidi ya dhambi katika asili yetu. Ni lazima tuache mapenzi yetu wenyewe na tamaa za dhambi. Mungu hutupatia nguvu tunapomtafuta kwa dhati na kumwamini, Na tunaposhinda, utukufu wote unamwendea.
Hakuna kitu kinachochukuliwa bila kupigana, lakini tunapopigana, hakuna kitu ambacho hatuwezi kuchukua. "maadui" mmoja baada ya mwingine wataanguka mbele yetu. Kisha hatutaona tu “matunda ya nchi” kwa mbali. Tutawaonja: upendo, furaha na amani. Nchi ya ahadi itakuwa yetu.