Tunaweza kubadilishwa kabisa!

Tunaweza kubadilishwa kabisa!

Ahadi kuu ambayo Mungu ametupa ni kwamba tunaweza kubadilishwa kabisa!

12/1/20166 dk

Na Ukristo wa Utendaji

Tunaweza kubadilishwa kabisa!

Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua katika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu." Warumi 12:2.

Je, inamaanisha nini kugeuzwa? Inamaanisha kubadilishwa - sio kidogo tu, lakini kubadilishwa kabisa. Na matamanio makubwa zaidi ya Mungu kwetu ni kwamba tunaweza kubadilishwa kabisa kutoka kuwa watu wenye asili ya dhambi hadi kushiriki asili Yake tukufu, kamilifu ya kimungu. Hii ina maana kwamba asili yetu, mawazo yetu na tabia zetu zinaweza kubadilishwa kabisa. Tunaweza kubadilika kutoka kuwa watu wenye dhambi, wenye huzuni hadi kujaa utukufu na wema wa Mungu! Hii ndiyo ahadi kubwa kuliko zote!

Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.” 2 Petro 1:4.

Je, tunabadilishwaje?

Kubadilika na kuwa kama Yesu Kristo (Warumi 8:29) kunagharimu kitu. Ili kushiriki asili ya kimungu sina budi kuacha asili yangu ya zamani. Ndiyo maana Yesu anasema kwamba “Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:14) Ni kwa sababu kuna wachache sana ambao wako tayari kuacha asili yao ya kale ya kibinadamu.

Utaratibu huu wa kubadilishwa utatokea katika maisha yangu yote. Ili kuanza mchakato huo, lazima kwanza nikiri kwamba asili yangu ya kibinadamu haina thamani, ni ya kutisha na imejaa dhambi. Lazima niwe na kilio moyoni mwangu, "Maskini mimi!" (Warumi 7:24) Ni lazima nifikie hatua ya kukiri kwamba siwezi kumtumikia Mungu jinsi ninavyofanya. Asili yangu haiwezi tu "kurekebishwa". Lazima niwe kiumbe kipya kabisa. (Wagalatia 6:15)

Na wakati nimeona kweli na kukubali kwamba hakuna kitu kizuri katika asili yangu ya kibinadamu (Warumi 7:18), basi niko tayari kuacha asili yangu ya zamani kwa kubadilishana na asili mpya. Kisha niko tayari kubadilishwa.

Na Mungu atanionesha jinsi gani.

Badiliko hili linakuja kidogo kidogo, kwa kila wakati kusema Hapana kwa dhambi inayokuja kutokana na asili yangu ya kibinadamu, kwa kutokubali hadi hamu ya kufanya dhambi hiyo kufa ndani yangu. Wakati wa siku yangu kuna hali tofauti tofauti ambazo napata kuona, kwa mfano, kutokuwa na subira, wivu wangu, hasira yangu, ubinafsi wangu, mashaka yangu, kiburi changu n.k Kwa kusema Hapana kwa mawazo haya ninapojaribiwa kwa dhambi hizi na sio kuyaruhusu kukua, yatakufa mwisho. (Wakolosai 3:5) Ninakataa mawazo hayo na kumwacha Mungu abadilishe sehemu yangu hiyo. Kila wakati ninapofanya hivi, mimi huchukua hatua kwenda mbele kwenye njia nyembamba.

Kwa hiyo wakati, kwa mfano, mawazo ya wivu yanakuja ndani yangu, basi naweza kusema Hapana. Kataa kuiacha ikue! Mawazo ya wivu ni tofauti na asili ya kimungu kama vile usiku ni tofauti na mchana! Kwa kweli inachukua muujiza kubadilishwa kutoka kukubaliana na mawazo kama haya ya dhambi hadi kupata asili ya kimungu katika eneo hili. Yanipasa kumlilia Mungu aniokoe na dhambi hii na sina budi kuomba kwamba anipe nguvu nisikubali kamwe kuwa na mawazo haya ya dhambi! Ninaomba kwamba atanibadilisha kabisa katika eneo hili.

Na Roho Mtakatifu hunipa uwezo wa kutokubali kamwe katika mawazo hayo ya dhambi. Na mwishowe, wakati "imekufa", Mungu hunipa kipande kidogo cha asili ya kimungu mahali pake. Hata katika hali zinazoonekana kuwa zisizo muhimu sana, ninaweza kushiriki katika ahadi hizo za thamani zaidi na kupata sehemu ndogo ya asili ya kimungu, uzima wa milele! Mungu anafanya muujiza ndani yangu. Ni kichocheo kama nini cha kuwa mwaminifu!

“Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa Imani yenu, ambayo ina thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekana kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.” 1 Petro 1:6-7.

Unaweza kubadilishwa kila siku

Kila siku kuna fursa nyingi kwangu za kubadilishwa. Lakini ikiwa sioni fursa hizi, ikiwa sioni dhambi ndani yangu na kuikataa, basi ninapoteza siku zangu na kuishi kila siku na lengo lisilofaa katika akili!

Huu utaratibu wa kubadilishwa sio kitu cha kichawi ambacho Mungu atakifanya siku moja nikiwa mkubwa ni jambo ambalo lazima lifanyike kila siku. Ikiwa mimi ni mtu yule yule leo kama nilivyokuwa jana, basi ninawezaje kutarajia kuwa mtu aliyebadilika kabisa mwishoni mwa maisha yangu? Je, umebadilika kutoka kuwa mbinafsi na mwenye dhambi, na kuwa mtu ambaye anashiriki asili ya kimungu?

Labda nisione leo kwamba mimi ni mtu tofauti sana na nilivyokuwa jana. Mara nyingi mabadiliko ni madogo. Na kuna njia ndefu ya kwenda. Lakini baada ya muda nitaona kwamba nimekuwa mvumilivu zaidi, kwamba nimekuwa mwenye upendo zaidi, kwamba nimekuwa mcha Mungu zaidi kuliko nilivyokuwa hapo awali, na hilo litanifanya kuwa na furaha sana! Ninaweza kutazama maisha yangu na kuona kwamba nyakati zote nilizosema Hapana kwa kutokuwa na subira kwa kweli kumesababisha kuwa rahisi kwangu kuwa mvumilivu sasa. Ninabadilika! Ninabadilika zaidi na zaidi!

Lengo tukufu la mwisho

Lengo langu la mwisho na maisha yangu ni kwamba nibadilishwe kadiri niwezavyo ili nifanane na Kristo - kwamba nimejazwa kadiri niwezavyo na asili ya kimungu. Kisha ninapokuwa na watu wengine, wanapata furaha na amani tu na upendo na subira kutoka kwangu.

Yesu alikuwa mwanadamu alipokuwa hapa duniani, na alijaribiwa kama mwanadamu mwingine yeyote, lakini alipigana na dhambi na hakukubali kamwe. Na angeweza kusema, "Wale walioniona mimi wamemwona Baba." ( Luka 2:52; Yohana 14:7-10; 1 Petro 4:1 ) Yesu hakukubali kamwe chochote ambacho kilitokana na asili yake ya kibinadamu na, kwa sababu hiyo, katika maisha yake matendo yake yote yalikuwa ya kimungu. Ndani yake vita dhidi ya dhambi vilikuwa vikiendelea, lakini watu waliomzunguka walimwona tu Baba ndani yake.

Hilo ni lengo langu pia! Hiyo ndiyo ninayotaka! Hiyo ndiyo hamu yangu ya pekee nikiwa hapa! Pia ninataka kusema: “Yeye ambaye ameniona mimi amemwona Baba.” Pia nataka kuja kwenye hali hiyo ya kimungu.

Na kwa neema ya Mungu hili linawezekana kweli.

Chapisho hili linapatikana katika

Makala hii ilichapishwa kwenye https://activechristianity.org/ na imebadilishwa kwa ruhusa ya matumizi kwenye tovuti hii.